
Rais Jakaya Kikwete akiwahutubia mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania
katika nchi za nje wakati wa ufunguzi rasmi wa mkutano wa siku tatu
ulioanza, Dar es Salaam juzi. Picha na Anthony Siame.
Dar es Salaam. Rais
Jakaya Kikwete amewaaga rasmi mabalozi 36 wa Tanzania katika mataifa
mbalimbali akiwaeleza kuwa hatakuwa madarakani baada ya Oktoba.
Rais aliwaaga mabalozi hao jana wakati akifungua mkutano wa siku tatu
utakaohitimishwa leo, ambao pamoja na mambo mengine, utajadili
‘Diplomasia ya Tanzania Kuelekea Dira ya Taifa 2025.’
“Huu ni mkutano wangu wa mwisho kuzungumza nanyi. Mmenisaidia vizuri
katika kipindi chote cha utawala wangu na niwaahidi tu kuwa nitaondoka
Ikulu baada ya uchaguzi mkuu ujao,” alisema Rais Kikwete.
Pamoja na kuaga, aliwaachia mambo manne ya kuzingatia ili kuifanya
Tanzania iendelee kuheshimika kimataifa. Mambo hayo yanajumuisha;
kuwasaidia wawekezaji wa Kitanzania kupata fursa katika nchi
wanazoziwakilisha; kuwasaidia Watanzania walioko katika nchi
wanakowakilisha kuunda umoja wao; kuzishawishi asasi za kiraia za
kimataifa kuja kuwekeza nchini pamoja na kutengeneza marafiki wa Taifa
kwa ujumla.
Rais alieleza kuwa wakati Serikali ikitekeleza mpango wa kuifanya
Tanzania kuwa nchi ya kipato cha kati ifikapo 2025, tayari kuna wananchi
wenye uwezo wa kiuchumi ambao wameshaanza kuwekeza katika baadhi ya
nchi Afrika na hata nchi za Magharibi, hivyo ni vyema wakapewa
ushirikiano wa kutosha ili kufanikisha azma zao.
“Niwakumbushe tu kuwa mahitaji yamebadilika nanyi pia badilikeni. Kwa
sasa ni vyema vipaumbele vyenu vikawa uwezo wa kuleta mitaji nchini,
kiasi cha misaada ya maendeleo mlichochangia, masoko kwa bidhaa zetu
mliyoyabainisha na wawekezaji wa nje mliowashawishi kuja kuwekeza,”
alisema Kikwete na kuongeza:
“Achaneni na ripoti zenu za kila mwisho wa mwezi mnazoleta za malalamiko
mara eeeh wanataka mabadiliko kwenye cyber crime (Sheria ya Makosa ya
Mtandaoni) au Sheria ya Takwimu. Hayo masharti wanayotoa ndiyo maana
ilifikia hatua nikasema kuwa kama hatuwezi kupata mikopo bila masharti
ni bora tusipewe tu.”
Rais pia aliwataka mabalozi hao kuzihoji serikali za nchi waliko juu ya
mchango wao katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ambayo athari
zake zinaziathiri sana nchi zinazoendelea kama Tanzania.
Alifafanua kuwa kama jotoridi la dunia litaendelea kuongezeka upo
uwezekano mkubwa ifikapo mwaka 2030 Mlima Kilimanjaro usiwe na theluji
iliyopo sasa, hali itakayopunguza mvuto wake na hivyo kuathiri utalii.
Alisema: “Ukame umeongezeka… mwaka jana hatukupata mvua kabisa za vuli.
Mazao yamekauka na ipo dalili kuwa kutakuwa na upungufu mkubwa wa
chakula mwaka huu.”
Aliongeza kuwa aliingia madarakani nchi ikiwa haina adui na anaondoka
nchi ikiwa hivyo pia na kuwakumbusha kuwa ni vyema kila mmoja
akajitahidi katika hilo.
Akimkaribisha Rais kufungua mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alisema kwa kipindi cha miaka 10
iliyopita nchi imeshirikiana vyema na mataifa mengi ulimwenguni jambo
lililowezesha kufunguliwa kwa Ubalozi wa The Hague pamoja na kufutiwa
madeni na ongezeko la misaada ya maendeleo.
Makamu Mwenyekiti wa
Kamati ya Kudumu ya Bunge, Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Mussa Azzan Zungu alimweleza Rais kuwa kamati yake imekuwa ikishirikiana
vyema na wizara kuifanya Tanzania iendelee kuwa na uhusiano mwema wa
kidiplomasia.
MWANANCHI
Chapisha Maoni