
Mkuu wa
Ofisi na Mwakilishi wa UNESCO nchini, Bi. Zulmira Rodgrigues,
akiwasilisha mada katika warsha ya siku tatu iliyofanyika katika kijiji
cha Nyakahungwa wilayani Sengerema mkoani Mwanza kuhusu ushirikishaji
jamii katika kuandaa na kutekeleza mikakati itakayochangia kuzuia na
kutokomeza unyanyasaji na dhulma zinazofanywa dhidi ya watu wenye
albinism iliyoshirikisha waganga wa asili, wauguzi na wakunga, viongozi
wa dini, walimu pamoja na watu maarufu iliyoandaliwa na Shirika la Umoja
wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).


(kilonge)






Mauaji ya
watu wenye ulemavu wa ngozi (albinism) yanayoendelea nchini yanatokana
na mitazamo hasi kitamaduni miongoni mwa wanajamii.
Hayo
yameelezwa na washiriki wa warsha ya siku tatu inayoendelea katika
kijiji cha Nyakahungwa kata ya Nyakahungwa wilayani Sengerema yenye
lengo la kubadili mitazamo iliyojengeka katika jamii na kusababisha
madhara makubwa kwa watu wenye albinism iliyoandaliwa na Shirika la
Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).
Warsha
hiyo ni miongoni mwa mlolongo wa warsha nne zitakazofanyika katika
wilaya za Sengerema, Mwanza, Kahama na Bariadi kwa kuzishirikisha jamii
kuibua masuala mbalimbali yanayobagua, kunyanyapaa na kuwatenga watu
wenye albinism katika maeneo husika.
Warsha
hizo zinafanyika katika kipindi ambacho kumetokea mauaji ya mtoto wa
kike, msichana na kijana wenye albinism wilayani Sengerema wakati tarehe
14 Mei 2015 mwanamke mmoja alikatwa mkono wilayani Bariadi.
Kwa
mujibu wa Afisa Maendeleo Jamii wilayani Sengerema Bwana Bushaija Vicent
kati ya shule za msingi 191 wilayani humo ni Shule zenye watoto wenye
albinism ni 14, Idadi yao ni 16 katika shule ya awali watoto 4 wana
albinisim, vyuo mbalimbali Sengerema vijana 4 wana albinism na katika
Shule za sekondari 48, watoto wenye albinism 4.
Akitoa
mada kuhusu uhamasishaji jamii katika masuala ya albinism, Mkuu wa Ofisi
na Mwakilishi wa UNESCO Bi Zulmira Rodgrigues amesema miongoni mwa
masuala ambayo warsha italenga ni kutafakari kwa kina kwa nini watu
wenye albinism wanauawa, kubaguliwa, kutengwa na mambo yanayosababisha
Tanzania kuongoza katika mauaji hayo ikilinganishwa na nchi nyingine
ambazo pia zina watu wenye albinism.
"Watu
wenye albinism hawauwawi katika sehemu nyingine duniani, kwa nini
Tanzania? Ikiwa mauaji hayo yako kwa wingi nchini Tanzania basi kuna
tatizo kubwa ambalo linatakiwa kufanyiwa kazi, na si serikali, UNESCO
wala taasisi yoyote ambayo inaweza kuleta mabadiliko hayo isipokuwa
jamii yenyewe," alisema Rodrigues.
Tatizo
kubwa lililotajwa kuhusiana na mauaji ya watu wenye albinism ni
utamaduni uliojengeka katika fikra za watu na kuwa na imani kwamba watu
wenye albinism si watu wa kawaida, hawana hadhi na hawastahili kuishi.
Watu
wenye albinism ni watu wa kawaida wanaostahili heshima na kulindwa kama
binadamu wengine kulingana na kanuni na sheria za nchi na za kimataifa
zinazopinga ubaguzi wa rangi, jinsia, tabaka na kukatisha maisha ya mtu.
Tofauti ni kwamba rangi yao inatokana na ukosefu wa vinasaba asili
vijulikanavyo kama melanin, vyenye uwezo wa kuzalisha rangi ya nywele,
macho na ngozi.
Utamaduni
uliojengeka katika jamii wa kuwabagua, kuwatenga na kuwapuuza watu
wenye ulemavu wa ngozi kumehalalisha mauaji ambayo kwa hivi sasa imekuwa
biashara ya kuuza viungo vya watu wenye albinism kwa waganga wa asili
kwa lengo la kupata utajiri, cheo na madaraka.
"Mara
nyingi waganga wa asili wamekuwa wakitajwa kuwa ndio chanzo cha mauaji
hayo kwa ajili ya imani potofu ya kujipatia utajiri, vyeo na madaraka.
Biashara hiyo inaonekana kushamiri kwa kuwa hakuna mifumo mahsusi
kudhibiti maafa hayo," alisema mmoja wa washiriki anayeshughulikia
masuala ya usalama.
Akichangia
mada wakati wa majadiliano yanayokusudiwa kuzalisha mikakati ya
kukomesha maovu hayo, Mratibu na Mkufunzi wa Redio Jamii kutoka UNESCO
Bi Rose Haji Mwalimu alisema kwamba wakati umefika wa kutambua kitu gani
kizuri katika tamaduni zilizopo zitakazoweza kusaidia kuleta mafanikio
na kuachana na zile ambazo hazina tija na zinasababisha maafa katika
maendeleo na ustawi wa jamii.
"Ni kweli
kuna changamoto nyingi katika jamii zinazosababishwa na kuhalalisha
tamaduni zinazolenga kupotosha badala ya kujenga. Tukiendelea
kuzikumbatia tutajikuta tunajenga taifa lisiloona mbali kimaendeleo
kuhadaiwa na watu wenye ubinafsi kutoka nje na ndio maana Tanzania
imekuwa soko kubwa au shamba lenye rutuba ya kupandikiza mbegu ambazo
mavuno yake hupatikana kwa urahisi", alisema Bi Mwalimu.
Katika
warsha hiyo washiriki walibaini maeneo makuu matatu ya kuyawekea mpango
kazi. Maeneo hayo ni Kuzuia mauaji, ubaguzi, unyanyapaa na kuwatenga,
eneo la pili ni kuwalinda watu wenye albinism katika maeneo ya makazi,
mashuleni, katika jamii na familia zao na la tatu ni hatua za kisheria
wale wote watakaoonekana kuhusika moja kwa moja au kwa namna nyingine
katika kuwatendea maovu watu wenye ulemavu wa ngozi kuanzia ngazi za
kimataifa, kitaifa, kifamilia na shuleni.
Chapisha Maoni