Katika
jitihada za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuboresha huduma kwa
wateja kama ilivyoainishwa kwenye Mkataba wa Huduma kwa Mteja, leo
Shirika la Nyumba la Taifa linazindua huduma mbili, ambazo ni kituo cha
huduma kwa wateja na pili ni mfumo wa kulipa kodi za nyumba kwa kutumia
simu ya kiganjani.
Kituo
cha huduma kwa wateja kwa njia ya simu kitatumika kuhudumia wateja wetu
wote kwa kupiga simu pale wanapohitaji kufahamu juu ya huduma zetu na
bidhaa mbalimbali pamoja na kutoa taarifa mbalimbali za shirika
zinazohusu huduma kwenye makazi yao.
Wateja wataweza kupata huduma hii kupitia nambari +255 784 105 200 na
+ 255 222 162 800. Kupitia kituo hiki Shirika linawaahidi kwamba
maulizo na taarifa zozote zitakazoripotiwa zitapewa kipaumbele kwa
kupatiwa ufumbuzi haraka iwezekanavyo.
Katika
kuendelea kuboresha mfumo wa ukusanyaji kodi kutoka kwa wapangaji wetu,
Shirika limeanzisha mfumo wa kulipa kodi kupitia simu za kiganjani ili
wapangaji waweze kufanya malipo ya kodi zao bila ya usumbufu wowote
kupitia tigopesa, mpesa na airtel money.
Kupitia
mfumo huu, wapangaji wataweza kufanya malipo kwa kutumia simu zao na
wataweza kuhamisha fedha kutoka kwenye benki akaunti zao na kwenda
Shirika la Nyumba mahali popote walipo na kwa muda wowote ambao ni
muafaka kwao bila ya kufika katika vituo vyetu vya makusanyo ya kodi.
Chapisha Maoni