0
Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi
MSAJILI wa Vyama vya Siasa Nchini, Jaji Francis Mutungi amevitaka vyama vya siasa na wagombea nchini kuzingatia Sheria ya Gharama ya Uchaguzi, kwani isipozingatiwa itawaathiri wengi watakaokiuka.
Alisema wote watakaokiuka, watajikuta wakikwamisha kuendelea na mchakato wa kusimamisha wagombea au wagombea wenyewe kuenguliwa, hivyo kusisitiza umakini katika kuizingatia Sheria hiyo iliyotungwa mwaka 2010 na ikitarajiwa kuanza kutumika mwaka huu.
Aidha, amevitaka vyama vya siasa ambavyo katiba zao zinaruhusu chama kuanzisha vikundi vya ulinzi na usalama kutambua kuwa vikundi vyao ni batili, kwani havitambuliwi na ofisi yake na hata Katiba, hivyo vivunjwe au kusitisha shughuli zake.
Jaji Mutungi alisema hayo jana wakati akizungumzia sheria ya gharama za uchaguzi pamoja na vikundi vyenye mwelekeo wa kijeshi kuwepo kwenye vyama vya siasa na kusema sheria itafuata mkondo kwa yeyote atakayebainika kukiuka sheria ya gharama za uchaguzi ndani na nje ya chama.
Alivitaka vyama kuhakikisha wanachama wake wanazingatia sheria hiyo, kwani wasipofanya hivyo kuna hatari ya mgombea wake kuwekewa pingamizi kwani sheria hiyo imeainisha wazi kuwa chama cha siasa ndicho kitagharimia mchakato wa kura ya maoni na kampeni za uchaguzi.
“Hii ni pamoja na gharama zote zitakazotumika katika uhamasishaji kwa lengo la kumnadi mgombea kwa wapigakura, gharama za chakula, vinywaji, malazi ama usafiri,“ alisisitiza.
Alisema kwa sasa ni vyema kuacha demokrasia itawale kwenye vyama kwa kufanya shughuli zake bila kuingiliwa ili kukuza demokrasia na itakapofika muda na watu kupeleka malalamiko na kuchunguzwa na taasisi husika wataweka pingamizi kwa jambo husika.
Alisema sheria inaelekeza kuwepo kwa uwazi katika mapato na matumizi ya vyama na wagombea wao kabla wakati na baada ya uchaguzi na kuweka utaratibu wa kudhibiti gharama za uchaguzi kwa kuweka viwango vya juu vya gharama hizo ambapo vimezingatia tofauti ya majimbo, idadi ya watu na miundombinu ya sehemu husika.
Msajili alisisitiza kuwa sheria inavitaka vyama vya siasa kuwa wazi kwa michango ya hiari na zawadi zinazotolewa kwa chama na wagombea na kuvitaka kufahamu kuwa sheria inakataza kufanya malipo kwa wapigakura ili kumchagua mgombea fulani, kuahidi kazi ama cheo, kutoa mikopo na ahadi ama makubaliano yoyote na mpigakura ili kumchagua.
“Kufanya vitendo vyovyote vyenye kuashiria kurubuni ama kushawishi wapigakura wakati wowote kabla au baada ya uteuzi wa mgombea ni ukiukwaji wa sheria kwani Tanzania ilianzisha sheria hii kwa dhamira ya kukuza na kuimarisha demokrasia nchini,” alisisitiza.
Alisema katika uchaguzi wa mwaka 2010 kabla ya kutungwa kwa sheria hiyo kulikuwepo na malalamiko mengi ya vitendo vya rushwa jambo lililoashiria kuwa kuna watu huchaguliwa kutokana na kuwashawishi wapigakura kwa kutumia fedha badala ya uwepo wao wa kuongoza na sera za vyama vyao.
“Natoa wito kwa wanaotarajia kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kujiepusha na vitendo vyovyote vinavyoonekana kuleta hisia za kununua ama kurubuni wapigakura kwani kufanya vitendo kinyume cha sheria kutamkosesha mgombea sifa za kugombea nafasi ya uongozi,” alisema.
Naye Msajili Msaidizi, Kitengo cha Gharama za Uchaguzi na Elimu kwa Umma, Princia Kiule alisema kwa mujibu wa sheria kifungu cha 14 katika mchakato wa uteuzi chama kinatakiwa kugharimia mchakato kwa kutumia gharama isiyovuka Sh bilioni mbili.
Vikundi vya ulinzi
Akizungumzia vikundi vyenye mwelekeo wa kijeshi katika vyama vya siasa alisema sheria ya nchi na ile ya vyama vya siasa zinapiga marufuku vyama viwe vimesajiliwa au la kuanzisha vikosi au vikundi vya ulinzi vinavyochukua jukumu la polisi au majeshi kwani jukumu la kutunza na kulinda amani katika shughuli za kisiasa linabaki kuwa la Jeshi la Polisi.
Mutungi alisema kisheria, Katiba na kanuni za vyama hazipaswi kupingana na sheria ya nchi hivyo ikiwa vyama vina ibara au kanuni zinazopingana na sheria ya nchi ibara au kanuni hiyo inakuwa batili.
“Kwa maana hiyo, ibara na kanuni za vyama zinazoruhusu chama husika kuanzisha vikosi hivi ni batili na havitambuliwi na ofisi yangu kama sehemu ya Katiba ya chama hata kama chama husika kimekataa kuondoa ibara hizo katika Katiba zao,” alisisitiza.
Alivitaka vyama vya siasa vyenye umiliki wa vikundi vya ulinzi na usalama na kuvipatia mafunzo ya kijeshi kwa kusingizia ulinzi wa mali na viongozi wao kuvivunja vikundi hivyo na kuacha mara moja mafunzo ya kijeshi, kwani ni kinyume cha sheria ya nchi.
Alisema wakati nchi inaelekea kwenye uchaguzi mkuu inahitajika amani na utulivu ili wananchi wapate nafasi ya kutafakari maamuzi ya kuchagua viongozi wao, kwani vikundi katika vyama kwa ajili ya kulinda mali na viongozi ilianza wakati wa mfumo wa chama kimoja na kuendelea hadi mfumo wa vyama vingi ulipoanza.
Alisema majukumu ya vikundi hivyo siyo kuchukua yale ya Jeshi la Polisi kama ilivyo sasa, bali kushirikiana na jeshi kama raia wema kutoa taarifa za uhalifu katika shughuli zao za kulinda mali na viongozi wa chama hivyo ofisi ya msajili haikuona tatizo la kuendelea na utaratibu huo mwaka 1992.
Lakini tofauti na matarajio ya awali vyama vinavyomiliki vikundi hivyo vimebadili mfumo, majina, uendeshaji na mwelekeo wa vikundi hivyo na kuwa na mfumo wa kijeshi na kuviita vikosi vya ulinzi na usalama wa vyama, kuainisha mafunzo maalumu ya ukakamavu, kujilinda na kupambana na hata kuweka vyeo kama jeshi jambo ambalo ni ukiukwaji wa sheria za nchi.(HABARI LEO)

Chapisha Maoni

 
Top