Na Mwandishi Wetu, Zanzibar.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Bernard Membe (pichani) , amenusurika kifo baada ya ndege
aliyokuwa akisafiria kutoka Iringa kwenda Zanzibar kutaka kugongana uso
kwa uso na ndege nyingine dakika moja kabla ya kutua.
Waziri Membe akiwa na ujumbe wake wa
watu wanane, walikuwa wakisafiria ndege ya kukodi kampuni ya 5H NEG
Precition Aviation ikirushwa na rubani Mathew Mhahiki, ambaye ameonyesha
kushangazwa na tukio hilo alilodai “ni kwa rehema za Mungu tumepona
ajali hii.”
Akizungumza na mwandishi wetu aliyeko
katika ziara yake, rubani Mhahiki alisema: “Lazima kuna tatizo katika
control center hata hivyo tayari nimeongea nao na wameniomba samahani na
kudai walipitiwa, maana kwa hali ilivyokuwa ni kwamba tungegongana
wakati wa kutua maana nimeshangaa tu kuona ndege hii hapa ndiyo maana
nikaamua kumkwepa mwenzangu nikapanda juu.”
Waziri Membe alisema: “Nina uzoefu
mkubwa wa kusafiri na ndege mahali pengi duniani, hali hii ilikuwa ni
ajali na labda sasa tungekuwa dead bodies, lakini ninajua Mungu yuko
upande wetu katika safari hii ya uhakika, lakini pia izingatiwe nimekuja
kufanya kazi ya Mungu.”
“Katika safari hii tutashuhudia mambo
mengi sana, lakini kwa kuwa kila ninapotaka kuondoka nyumbani ama
hotelini mara nyingi nimekuwa nikimtanguliza Mungu maana bila Mungu hii
ilikuwa ni mwisho wa maisha yetu tuliokuwa kwenye ndege hii.”
Waziri Membe alikuwa amealikwa mjini
hapa na Umoja wa Akimama wa Kikristu (Umaki) wa Kanisa la Anglikana
Dayosisi ya Zanzibar waliokuwa wakifanya mkutano wao mkuu unaofanyika
kila baada ya miaka mitano akitokea Iringa ambako alikwenda kutafuta
udhamini wa chama ili kumwezesha kugombea urais kupitia Chama Cha
Mapinduzi, CCM.
Akiwa uwanjani hapo, Waziri Membe
alikutana na Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba aliyekuja hapa
Zanzibar kutafuta wadhamini ambapo makada hao walipata nafasi ya
kuzungumza.
Akiwa katika mkutano huo, Waziri Membe
alisema: "Miongoni mwa mambo yanayonikera ndani nafsi yangu ni kuona
mwanamke bado anaachwa nyuma, hili halipendezi, ni lazima tuhakikishe
wanawake wanapata elimu ya ufundi stadi maana mwanamke akiwezeshwa hasa
katika eneo hili la elimu wanaweza hata kushinda wanaume wengi.”
“Ni lazima kina mama wawezeshwe
kujiajiri ili msiwategemee kina baba kwa kila jambo lakini pia ili
kufikia malengo hayo ni lazima tuwape elimu kina mama.”
Chapisha Maoni