
Baada ya
kumbwaga Mphilopino Many Pacquiao, bondia ambaye hajaonja ladha ya
kipigo katika mchezo wa masumbwi, Floyd Mayweather Jr amethibitisha
kupanda tena ulingoni Septemba 12 mwaka huu katika pambano linalotaraji
kufanyika mjini Las Vegas Marekani.Mayweather ambaye ameshinda mapambano
48 aliopanda ulingoni bila sare wala kupoteza akishinda mapambano 26
kwa ‘knockout’, anashikilia mataji ya WBC na WBA katika uzito wa
‘welter’ alidhihirishia ulimwengu ubora wake kwa kumtwanga kwa wingi wa
alama mpinzani wake Many Pacquiao katika pambao lilivunja rekodi ya
mapato katika mchezo wa ngumi ulimwenguni.
Mmarekani huyo aliyepokonywa mkanda wa
WBO baada ya kukiuka masharti mapema wiki hii, ametuma ujumbe kwenye
mtandao wa kijamii ukiashiria kurudi kwake ulingoni kabla ya kuisha kwa
mwaka huu.“Kwa mashabiki wangu. Uaminifu wenu na sapoti yenu vimenipa miaka 20 bora ambayo ningeiomba. Na nikiwa juu, napanga kwenda juu. Tukutane tena ulingoni Septemba 12,” ulisomeka ujumbe wa Mayweather.
Taarifa hizo zinaweza kuibua fununu nyingi juu ya nani atavaana na bondia huyo katika pambano hilo kwani mabondia kadhaa wameshatajwa kupanda naye ulingoni akiwemo Andre Berto aliyeshinda mapambano 30 na 23 kwa ‘knockout’ pamoja na Karim Mayfield aliyeshinda mapambano 19 huku 11 kati ya hayo akimaliza kwa ‘knockout.’
Mwingine anayevumishwa kupanda ulingoni na bingwa huyo ni bingwa wa zamani wa dunia Amir Khan ambaye kwa kipindi kirefu amekuwa akisaka nafasi ya kuzichapa na Mayweather bila mafanikio lakini itawabidi wapenzi wa ndondi kusubiri mpaka itakapotangzwa rasmi ni bondia gani atakwenda kuendeleza au kuvunja rekodi ya nguli huyo wa mchezo wa masumbwi ulimwenguni kwa sasa.(VICTOR)
Chapisha Maoni