0
WAZAZI wa wanafunzi wanaosoma shule za msingi Mgongo na Kigonzile, Kata ya Nduli manispaa ya Iringa wamempongeza Diwani wao, Bashir Mtove kwa kusimamia ujenzi wa vyoo ambavyo vilikuwa vikitishia afya ya watoto wao.
Wakizungumza na Uhuru, wazazi hao walisema kwa kipindi kirefu shule hizo zilikuwa zikikabiliwa na uhaba mkubwa wa matundu ya vyoo jambo ambalo lingeweza kusababisha magonjwa ya mliuko.
Walisema kuna wakati wanafunzi wa shule hizo walikuwa wakilazimika kuingia maporini kutokana na uhaba huo.
Mkazi wa Kigonzile, Abibedi Kanywaga alisema tangu kuchaguliwa kwa diwani huyo katika uchaguzi mdogo, uliofanyika mwaka mmoja uliopita, ujenzi wa vyoo vya shule umeenda kwa kasi kutokana na usimamizi wa karibu.
Diwani wa kata hiyo, Mtove alisema kutokana na tatizo kubwa la uhaba wa matundu ya vyoo shuleni hapo aliamua kuita mkutano wa wazazi, na kuwashirikisha namna gani watatatua changamoto hiyo.
Alisema kwa kushirikiana na wananchi wake, walipata fedha kidogo toka kwa wafadhili mbalimbali ikiwemo serikali, na kuamua kuunganisha nguvu zao kuanza ujenzi wa vyoo hivyo.
Alifafanua kuwa kwa muda mfupi ujenzi wa vyoo ulikamilika na kwamba, shule hizo ni kati ya shule zenye vypoo bora kwa manispaa nzima ya Iringa kiasi ambacho huzilazimu shule nyingine kwenda kujifunza.
Mbali na ujenzi wa vyoo hivyo, Mtove alisema ameanza kushughulikia tatizo la baadhi ya maeneo kukosa shule na hivyo kuwalazimu wanafunzi kutembea umbali mrefu kwa ajili ya kufuata masomo.
Aliyataja maeneo hayo kuwa ni Kipululu ambako wanafunzi hutembea umbali wa kilometa 14, kufuata shule iliko na Msisima ambako wananchi wake hutembea umbali wa kilometa 12.
Kutokana na umbali huo alilazimika kuwashawishi, wazazi kujenda darasa moja ambapo mwaka huu wanafunzi wa darasa la kwanza, wameanza kusoma kwenye maeneo yao na kuwa ujenzi wa shule unaendelea.

Chapisha Maoni

 
Top