KAMATI ya
Baraza la Wawakilishi ya Katiba na Utawala Bora, imempongeza Rais
Jakaya Kikwete kwa kumaliza mgogoro wa kisiasa na kuimarika kwa amani na
utulivu chini ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Hayo
yalisemwa na Mjumbe wa Kamati ya Ofisi ya Kusimamia Viongozi Wakuu wa
Serikali, Shadya Mohamed Suleiman wakati akisoma maoni ya kamati hiyo
katika hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Rais, Ikulu na Utawala bora.
Suleiman
alisema wakati Rais Kikwete alipoingia madarakani alisema anasononeshwa
na mgogoro wa kisiasa uliopo Zanzibar na kusema ataufanyia kazi kwa
kuupatia ufumbuzi wa kudumu.
Alisema
kazi iliyofanywa na Rais Kikwete ni kubwa, ambapo mazungumzo ya kumaliza
mgogoro wa kisiasa Zanzibar, yalianza na hatimaye Serikali ya Umoja wa
Kitaifa iliundwa na kufanya kazi zake vizuri hadi leo.
"Tunampongeza
Rais Jakaya Kikwete kwa kazi kubwa ya kufanikisha kuleta amani ya
kudumu ya kumaliza mgogoro wa kisiasa na hatimaye kuundwa kwa Serikali
ya Umoja wa Kitaifa," alisema.
Alisema
Rais Kikwete atakumbukwa kwa kazi hiyo wakati akimaliza muda wake wa
kipindi cha miaka 10 cha urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mwakilishi
wa Jimbo la Kiwani, Hijja Hassan Hijja (CUF) alisema akiulizwa jambo
gani lililofanywa na Rais Kikwete, ambalo hatalisahau katika maisha yake
ni uwezo wake wa ushawishi wa kumaliza mgogoro wa kisiasa Zanzibar.
Hijja
alisema Kikwete anastahiki kupongezwa kwa sababu ya kufanya kazi kubwa
ya kumaliza mgogoro wa kisiasa Zanzibar, ambao ulikuwa ukichafua jina la
Tanzania kama kisiwa cha amani na utulivu mkubwa.
Alisema,
leo hii tunashuhudia wananchi wanaishi kwa pamoja na kushirikiana pamoja
na kufanya kazi za kuleta maendeleo, kama ilivyokuwa zamani, kutokana
na kuunganishwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
"Mheshimiwa
Naibu Spika... mimi nikiulizwa jambo kubwa lililofanywa na Rais Kikwete
ambalo sitalisahau ni suala la kumaliza mgogoro wa kisiasa Zanzibar na
wananchi kuishi kwa amani na utulivu," alisema.
Chapisha Maoni