Wafugaji kutoka nchi za jirani waliovamia katika eneo la Loliondo wametakiwa kuondoa mifugo yao mara moja ili kuliacha eneo hilo kubaki na amani.
Akizungumza na wananchi na wafugaji wa kijiji cha Ololosokwani, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu alisema wakazi wa Loliondo wanauwezo wa kutatua migogoro yao wenyewe ila wanaosababisha migogoro hiyo isiishe na kuibuka mara kwa mara ni wageni wanaoingia katika eneo hilo na kuchungia mifugo yao.
“Ninatoa tahadhali kwa wageni wanaoitazama loliondo kwa jicho la husda waache kufugia mifugo yao loliondo, kila mmoja afugie kwao ardhi ya loliondo ni ya wana loliondo na sio wageni” alisema Nyalandu.
Alisema changamoto kubwa inayoikabili eneo hilo la Loliondo ni ongezeko la watu na mifugo wakati ardhi ikibaki kuwa ile ile. Nyalandu alisema kuna haja ya kuendeleza uhifadhi ili eneo
la Loliondo liendelee kustawi na wageni waendelee kuja Loliondo ambapo watachangia utalii endelevu katika shughuli kama za utalii wa picha na uwindaji.
Akizungumzia kuhusu miradi ya maji aliyoikabidhi kwa wananchi wa loliondo jana kutoka kwa Balozi wa Falme za Kiarabu waliofadhiri ujenzi wa miradi hiyo iliyogharimu sh bilioni 1.6 Waziri Nyalandu alisema hayo ni matunda ya ushirikiano mzuri baina ya Rais Jakaya Kikwete na Mfalme wa Dubai Shekh Makthum na Jumuiya ya falme za kiarabu.
Alisema utekelezaji wa miradi hiyo ni ahadi ya Rais Kikwete kwa maeneo ya wafugaji ambapo alisema azma yake ni kuona tatizo la maji katika maeneo ya wafugaji linamazika na kuona mifugo na wafugaji wakinenepa. Aliwataka wananchi wa Loliondo kuitunza miradi hiyo kwa faida yao na mifugo yao huku wakitumia muda mwingi kwa kazi za maendeleo ya loliondo.
Chapisha Maoni