0
 














SERIKALI imewashauri wananchi kutotumia mifuko ya plastiki na vifungashio vyake kuwekea au kuhifadhia chakula cha moto, kutokana na madhara makubwa ya kiafya, yanayoweza kutokea kwao.

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Stephen Masele alitoa hadhari hiyo jana bungeni na kutaka jamii itumie vifungashio vya glasi, chuma isiyoshika kutu na vyombo vingine vya asili, kama vile vibuyu.

Hadhari hiyo ya serikali imekuja wakati ambao wakazi wengi, hususani wa mijini, hutumia mifuko hiyo kuhifadhia vyakula mbalimbali vinavyoandaliwa haraka na zaidi, ikiwa viazi vya kukaanga maarufu kama chipsi.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri, madhara yanayoweza kusababishwa na uwekaji wa chakula cha moto katika mifuko ya plastiki ni kuwepo kwa uwezekano wa kemikali, zilizotumika kutengeneza mifuko hiyo kuingia kwenye chakula na kukifanya kuwa na sumu.
Sumu hiyo inaweza kusababisha saratani, kuharibu ukuaji wa mfumo wa uzazi hususani kwa watoto ambao hawajazaliwa, mabadiliko ya kijenetiki, matatizo ya kushindwa kuona, uyeyushaji wa chakula tumboni kuwa taabu au kutokamilika na ini kushindwa kufanyakazi vizuri.
Magonjwa mengine ni pamoja na kuharibika kwa mfumo wa utendaji wa figo na magonjwa yanayohusiana na mfumo wa kupumulia.

Naibu Waziri alisema hayo akijibu swali la mbunge wa viti maalumu, Mkiwa Adam Kimwanga (Chadema) aliyetaka kupata kauli ya serikali kuhusu mifuko ya plastiki na uchafuzi wa mazingira na madhara yanayoweza kusababishwa na uwekaji wa chakula katika mifuko hiyo.

Masele ambaye pia alijibu swali la nyongeza kutoka kwa mbunge wa viti maalumu, Christowaja Mtinda (Chadema) aliyetaka kufahamu ni lini serikali itafunga viwanda vya plastiki, aliwataka wananchi kushiriki kupiga vita mifuko hiyo watu wasiitengeneze au kuingiza nchini kinyemela.
Naibu Waziri huyo alisema serikali inatambua kuwepo kwa uchafuzi wa mazingira, unaotokana na matumizi ya mifuko ya plastiki nchini.

Alitaka kila mwananchi mwenye taarifa ya mahali inapotengenezwa mifuko hiyo midogo, ambayo tayari serikali na viwanda nchini, walishakubaliana kutotengenezwa, aitoe.
Alisema mifuko hiyo laini, yenye unene wa chini ya maikroni 30, ilishapigwa marufuku na akataka wananchi kuachana nayo kutokana na madhara yake kiafya.

Hata hivyo, alisema serikali kupitia Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC inaendelea na kufanya ukaguzi kwa kampuni, maduka na viwanda vinavyozalisha na kusambaza mifuko ya plastiki nchini kujiridhisha kama vinaizingatia sheria.

Zanzibar ilipiga marufuku utumiaji wa mifuko ya plastiki chini ya maikroni 100 mwaka 2005.
Anayekamatwa na mifuko iliyo chini ya maikroni hizo, hutozwa faini ya dola za Marekani 2000 au kifungo cha miezi au vyote viwili. Uganda, Kenya na Rwanda pia zimepiga marufuku matumizi ya mifuko yaplastiki chini ya maikroni 100.

Chapisha Maoni

 
Top