Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe
Dar es Salaam. Siku
mbili baada makada waliokuwa wamefungiwa kwa makosa ya kukiuka kanuni za
CCM kuachiwa huru, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Bernard Membe ameeleza nia yake kuwa wakati ukifika atachukua fomu
kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Membe alibainisha nia hiyo kwa mara ya kwanza juzi usiku wakati
akihojiwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC1) na kuwa atatangaza
azma hiyo muda wowote kuanzia sasa akiwa jimboni kwake, Mtama mkoani
Lindi.
“Sasa ni rasmi kuwa nina nia ya kugombea urais wa Jamuhuri ya Muungano
wa Tanzania. Nitatangaza nikiwa kijijini kwangu… mahali nilipoanzia
safari ya kwenda shule, safari ya kwenda usalama wa Taifa na safari ya
kwenda Wizara ya Mambo ya Nje,” alisema.
Membe alikuwa miongoni mwa makada sita CCM waliokuwa wamefungiwa kwa
takriban miezi 17 kwa makosa ya kukiuka kanuni za uchaguzi wakituhumiwa
kuanza kampeni mapema kinyume na taratibu za chama hicho kilicholazimika
kuwachukulia hatua za kinidhamu.
Makada hao walifungiwa tangu Februari, 2014 na pamoja naye ni mawaziri
wakuu wa zamani; Frederick Sumaye na Edward Lowassa; Waziri wa Kilimo,
Chakula na Ushirika, Stephen Wasira; Naibu Waziri wa Mawasiliano,
Sayansi na Teknolojia, January Makamba na Mbunge wa Sengerema, William
Ngeleja.
Akifafanua juu ya dalili za kutimia kwa ndoto yake za kuiongoza nchi,
Membe alisema Mwenyezi Mungu ana namna nyingi za kufikisha ujumbe kwa
mja ampendaye katika kumtumikia kwa mtindo autakao yeye. “Nimegundua
kuwa unaposema naomba nioteshwe… naomba nioteshwe kumbe Mungu anayo
namna nyingine. Anawaotesha wengine kwa ajili yako na ndivyo
alivyofanya,” alisema.
Kuhusu hilo, Membe alisema kila mtu anasubiri kuona CCM inatoka vipi na
hata vyama vya upinzani vinasubiri hilo na ndiyo maana navyo
vimenyamaza.
Mpaka sasa ni chama cha Tanzania Labour (TLP), kilichokwisha teua mgombea wake wa urais katika uchaguzi huo, Macmillan Lyimo.
“Watanzania wote macho yao yapo CCM, wanasubiri kuona inafanya nini.
Tunaona vyama vya vingine vimekaa kimya, wanasubiri CCM iseme ili nao
wafuate. Wanapiga kelele za Ukawa…Ukawa lakini hawawezi kufanya
chochote. Hata kama tutasogeza muda mbele bado wataendelea kusubiri,”
aliongeza.
Hali ya usalama Burundi
Waziri huyo pia alitumia nafasi hiyo kuzungumzia hali ya usalama
inayoendelea kuyumba nchini Burundi kwamba kikao cha mawaziri
kinatarajia kuketi baada ya muda mfupi jijini Arusha ili kuona namna ya
kutatua mzozo uliopo.
Alisema Tanzania isingekwa radhi kuona mapinduzi ya utawala wa Rais
Pierre Nkuruzinza yanafanywa wakati akiwa nchini tena kwa mwaliko na
gharama za nchi hii. Alisema hiyo ingemaanisha Tanzania inahusika nayo.
“Hilo haliwezi kufanyika kwa nchi hii. Tulilazimika kumrudisha na kama
wanataka kufanya mapinduzi wayafanye wote wakiwa huko. Tanzania siyo
nchi ya kuichezea na tusingeweza kukubali kuona hilo linatokea.
Alitanabaisha utata uliojitokeza baada ya Rais Nkuruzinza kutaka
kugombea tena muhula wa tatu kuwa ulishafafanuliwa na mahakama nchini
humo ambayo ilimruhusu kugombea.
“Tuliposuluhisha mgogoro wao wa awali, Bunge lao la mpito liliridhia
kuwa Nkurunziza aiongoze nchi hiyo mpaka uchaguzi mkuu utakapofanyika.
Aliiongoza Burundi kwa miaka mitano uchaguzi ukafanyika na akachaguliwa.
Katiba ya nchi hiyo inatoa muda wa miaka 10 kwa kiongozi mmoja lakini
kwa yeye miaka mitano haikutokana na kuchaguliwa, ndiyo maana
aliruhusiwa na Mahakama,” alisema.
Alifafanua pia kuwa usalama wa kila nchi ni muhimu kwa mustakabali wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na hiyo ndiyo maana wakuu wa nchi hizi
walilaani mapinduzi hayo punde tu yalipofanyika wakati wakuu hao
wakikutana nchini.
Akifafanua kuhusu mchakato wa kusuluhisha pande mbili zinazokinzana
nchini humo, Membe alisema iwapo mawaziri watashindwa kupata suluhu
katika kikao kinachotarajiwa kufanyika, watalazimika kumshauri
Mwenyekiti wa EAC, Rais Jakaya Kikwete hatua zaidi za kushughulikia
amani ya nchi hiyo.
Hadi sasa makumi ya wananchi wameuawa tangu kuanza kwa vurugu nchini
Burundi huku maelfu ya wakimbizi wakikimbilia Tanzania, Rwanda na
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC).
Mwananchi
Chapisha Maoni