Waziri wa nchi ofisi ya rais (kazi maalumu) Prof Mark
Mwandosya(picha kutoka Maktaba)
Serikali imeuondoa muswaada wa sheria ya
haki ya kupata habari 2015 uliokuwa uwasilisilishwe na kujadiliwa katika
mkutano unaoendelea wa bunge mjini Dodoma ili kutoa nafasi kwa wadau kutoa
maoni yao.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (asiye na wizara maalum) Prof Mark Mwandosya
ameliambia bunge leo asubuhi kuwa serikali imefikia uamuzi huo kutokana na
maoni ya kamati ya kudumu ya bunge ya maendeleo ya jamiii iliyotaka musawada
huo uondolewe ili kutoa muda wa kujadiliwa na wadau.
Katika taarifa yake hiyo kwa Bunge Mh. Mwandosya amewataka wadau
wa habari waendelee kutoa ushauri juu ya muswada huo pamoja na kuchangia maoni
zaidi ili kupata muswada ulio bora zaidi.
Prof Mwandosya amesema muswada huo utawasilishwa na kujadiliwa
katika mkutano ujao wa bunge ambao utakuwa ni wa bunge la kumi na moja chini ya
serikali ya awamu ya tano.
Uamuzi huo wa serikali umekuja kutokana na muswada huo kuzusha
mgogoro na wadau wa tasnia ya habari baada ya kuonekana kutowashirikisha wadau
wa habari moja kwa moja lakini pia kuonekana inaminya uhuru wa wananchi kupata
habari.
Wadau mbalimbali wa habari wakiwemo chama cha wamiliki wa vyombo
vya habari MOAT wamekuwa wakilalamikia maudhui ya muswada huo kwa madai ya
kuminya uhuru wa vyombo vya habari pamoja na haki ya kupata taarifa kwa
wananchi.
Katika mahojiano na mwanachama wa MOAT ambaye ni mwanzilishi
mwenza wa mtandao wa Jamii Forums jana (Juni 25) kupitia kipindi cha HOT MIX
cha EATV Maxence Melo, alisema kuwa endapo muswada huo ungepitishwa na kuwa
sheria, basi tasnia nzima ya habari ingekufa kwa kuwa umeweka njia ngumu ambazo
hazitekelezeki katika upatikana wa taarifa pamoja na mlolongo wa adhabu kali
kwa wadau na waandishi watakaokiuka sheria hiyo.
Naye mwanasheria na mtafiti wa uchumi na biashara kutoka katika
kituo cha sheria na haki za binadamu Masud George kupitia kipindi hichohicho
cha HOT MIX alisema kuwa muswada huo ni hatari kwa uchumi wa nchi kwani
shughuli nyingi za kiuchumi zinategemea upatikanaji wa taarifa sahihi na kwa
wakati.
Aliongeza pia kuwa, vyombo binafsi vya habari kama sehemu ya
wawekezaji katika sekta binafsi na chanzo muhimu cha ajira wanachangia kiasi
kikubwa cha uchumi wa nchi hivyo kuwadhoofisha ni kudhoofisha uchumi wa nchi
kiujumla.
Chapisha Maoni