
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Agnes Kijazi (mwenye suti nyeusi) akiongoza ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano Mkuu wa 17 wa Shririka la Hali ya Hewa Duniani unaofanyika Mjini Geneva, Uswisi. Wengine katika picha ni Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje, Balozi Celestine Mushy (Kulia)
TANZANIA YACHAGULIWA KUWA MJUMBE KATIKA BARAZA LA UTENDAJI (EXECUTIVE
COUNCIL) LA SHIRIKA LA HALI YA HEWA DUNIANI–WORLD METEOROLOGICAL
ORGANIZATION (WMO).
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Agnes
Kijazi, amechaguliwa kuwa Mjumbe katika Baraza la Utendaji (Executive
Council) la Shirika la Hali ya Hewa Duniani–World Meteorological
Organization (WMO) kwa kipindi cha miaka minne kuanzia 2015 hadi 2019.
Dr. Kijazi amechaguliwa tarehe 4 June 2015 wakati wa Mkutano Mkuu wa
Kumi na Saba wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO-Congress wa 17)
ulioanza tarehe 25 Mei 2015 na unatarajiwa kumalizika tarehe 12 Juni,
2015 Jijini Geneva, Uswisi.
Kuchaguliwa kwa Dr. Agnes Kijazi kumetokana na jitihada zilizofanywa na
Ubalozi wetu wa Kudumu Umoja wa Mataifa wa Geneva na Idara ya
Ushirikiano wa Kimataifa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa ambazo kwa pamoja zilisimamia zoezi la kuomba kura kutoka kwa
wanachama na kampeni wakati wa uchaguzi.
Dr. Kijazi ambaye anaongoza ujumbe wa Tanzania katika ushiriki Mkutano
huo ambao una washiriki kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Wizara ya Maji na Ubalozi
wa Tanzania Nchini Uswisi.
WMO ni Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya hali ya
hewa duniani na mabadiliko ya tabianchi. WMO inatekeleza majukumu na
maamuzi kuhusu maendeleo ya sayansi ya hali ya hewa na uboreshaji wake
ikiwa ni pamoja na kusimamia viwango katika upimaji na utoaji wa huduma
za hali ya hewa kwa nchi wanachama.
Hadi wakati wa Mkutano huu huko nchini Uswisi, WMO ilikuwa na nchi
wanachama 191. Katika Mkutano huu nchi za Sudan Kusini na Tuvalu
zilikaribishwa rasmi kama wanachama wapya wa WMO. Kati ya nchi hizi 191
ni nchi 37 tu ambazo zina wajumbe katika Baraza hilo kuu. Hivyo hii ni
nafasi adhimu na heshima kwa Tanzania, TMA na Dr Kijazi ambaye ni msomi
mwenye utaalamu wa kutosha akiwa na Shahada ya Uzamivu (Ph.D) katika
Sayansi ya Hali ya hewa.
Kazi kuu ya Baraza la Utendaji la WMO, ambalo Tanzania imefanikiwa kuwa
mjumbe ni kuchukua hatua zinazostahili, kwa kushirikiana na Katibu Mkuu
wa Shirika hilo kutekeleza maamuzi yanayotolewa na Mkutano Mkuu
(WMO-Congress) ambao hukutana mara moja kila baada ya miaka minne.
Akizungumza baada ya uchaguzi huo Balozi Celestine Mushy, Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa alielezea sababu ya
Tanzania kugombea nafasi hiyo muhimu kuwa ni pamoja na kuwa ndani ya
chombo cha maamuzi na hivyo kushawishi maamuzi yatakayoinufaisha jamii
nzima ya kimataifa ikiwemo Tanzania katika masuala ya hali ya hewa ikiwa
ni pamoja na kutoa mwelekeo wa kisayansi katika kukabiliana na athari
za mabadiliko ya hali ya hewa yanayoendelea katika maeneo mengi
Duniani.
Kwa upande wake, Dkt. Kijazi alieleza kuridhishwa kwake na jinsi ambavyo
nchi wanachama 190 walivyoridhishwa na utendaji wa Tanzania katika
kipindi cha miaka mitatu (2012-2015) ambacho alikuwa mjumbe wa Baraza
hili na hivyo kumchagua tena katika kipindi kingine cha miaka minne.
“Hii ni heshima kubwa kwa nchi yangu ya Tanzania na ninaahidi kutumia
uwezo wangu wote kutekeleza majukumu ya nafasi hii” alisema Dkt. Kijazi.
Imetolewa na: Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dar es Salaam
05 Juni, 2015
Chapisha Maoni