SPIKA wa
Bunge jana alilazimika kuahirisha shughuli za Bunge kutokana na baadhi
ya wabunge kukataa miswada mitatu isisomwe na kujadiliwa kwa pamoja
chini ya hati ya dharura.
Wakati
Spika akisema kuwa utaratibu huo ni wa kawaida na umekuwa ukifuatwa
kwenye vikao vingine vya Bunge vilivyopita, Kambi ya Upinzani ilikataa
maelezo hayo, kwa madai kuwa ni ukiukwaji wa kanuni unaolenga kufunika
kombe ili mwanaharamu apite.
Mara
baada ya kipindi cha maswali na majibu kuisha saa 4:00 asubuhi jana,
Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika aliomba mwongozo wa Spika,
akieleza kuwa, karatasi yenye maelekezo ya shughuli za Bunge jana
ilikuwa imebebanishwa miswada mingi kinyume na taratibu.
Mnyika
alianza kwa kusoma kanuni kadhaa, na kuulizwa na Spika alikuwa akitaka
nini kati ya mwongozo au taarifa, kwa sababu hakueleza kama anavyopaswa
kufanya, ndipo aliposema; “Ninaomba mwongozo, na ninautaka sasa hivi,
wala sio wakati mwingine, kwa sababu, inavyoonekana katika orodha ya
miswada kwenye karatasi hii (aliionesha) ya shughuli za Bunge (order
paper), imebebanishwa minne ifanyiwe kazi kwa wakati mmoja, jambo ambalo
ni tofauti na ukiukwaji wa kanuni”, alisema.
Miswada
iliyokuwa kwenye orodha ya shughuli za Bunge jana ni Muswada wa Sheria
ya Petroli wa Mwaka 2015, Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Mapato ya
Mafuta na Gesi wa Mwaka 2015, Muswada wa Sheria ya Uwazi na Uwajibikaji
katika Tasnia ya Uchimbaji Tanzania wa Mwaka 2015.
Kutokana
na hali hiyo, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema) alisimama kuomba
muongozo kwa sababu katika orodha ya shughuli hizo ilionesha kuwa baada
ya maswali na majibu kulikuwa na miswada ya serikali, ambapo ilionesha
ni kusomwa kwa mara ya pili na kusomwa mara ya tatu.
Alisema
miswada ya mafuta iliwasilishwa kwa hati ya dharura, hivyo kudai kanuni
zimekiukwa, jambo ambalo Spika Makinda alilipinga na kusema hakuna
kanuni iliyokiukwa, hali iliyofanya wabunge wa upinzani kusimama na
hivyo Spika kusitisha shughuli hizo.
Mnyika
alisema, “Pamoja na kuletwa kwa hati ya dharura ifanyiwe kazi yote leo
hii (jana), hatua hiyo inakiuka makubaliano ya kamati ya uongozi
iliyokaa Juni 29, katika ukumbi wa Msekwa katika viwanja vya Bunge
hili”.
Alisema
kilichotakiwa ni kukamilisha shughuli ya kupitisha au kutopitisha
muswada wa Kuwalinda watoa Taarifa za Uhalifu na Mashahidi, ulioachwa
kiporo juzi, ndipo kazi nyingine zifuate.
Akijibu
hoja yake, Spika Makinda alisema: “Kwanza ninaomba ufute kauli yako ya
kuniamrisha nikupe mwongozo leo hii kwa sababu huna mamlaka ya kufanya
hivyo, vinginevyo sitajibu kitu, nitakaa kimya”.
Mnyika
alifanya kama alivyoelekezwa na ndipo Spika alipojibu kuwa kinachofanywa
katika kikao hicho cha Bunge si uvunjaji wa kanuni, bali ni utaratibu
ambao umekuwa ukifuatwa hata kwenye vikao vingine vya Bunge hilo.
“Kinachoonekana
kwenye karatasi hiyo ni miswada na itafanyiwa kazi mmoja baada ya
mwingine kama kawaida. Hakuna kanuni iliyo vunjwa hapo na hakuna
ukiukwaji wa makubaliano uliofanyika,” Makinda alisema na ndipo Lissu
aliposimama kama Mnyika na kuwaonesha ishara ya kusimama wabunge wengine
wa upinzani, ambao walitii.
“Kutokana
na vurugu hiyo ya muda mfupi na majibishano yaliyomchukiza Spika
aliamua kusema: Nina ahirisha kikao hiki hadi baadaye,” alisema Spika.
Bunge lilirejea tena jioni na kuendelea kupitisha muswada wa kuwalinda watoa taarifa.
Wakati
Spika akitoka nje, baadhi ya wabunge wa upinzani walisikika wakitoa
maneno kuwa safari hii hawatatoka nje ya Bunge kuwapa mwanya wengine
waendelee kujadili miswada, bali watakuwepo ndani ya ukumbi huo wakiwa
wamesimama tu kuzuia chochote kisiendelee bila kufikia makubaliano.
Rage atoa tuhuma nzito
Mbunge
Tabora Mjini, Ismail Rage (CCM) aliwatuhumu baadhi ya wafanyabiashara wa
madini, mafuta na gesi kwamba wameingiza mkono katika suala la miswada
ya mafuta na gesi kwa kuwatumia baadhi ya wabunge ili miswada hiyo
isiwasilishwe bungeni, huku serikali ikisema ikikwama ni hasara kwa
Watanzania.
Rage
alitoa kauli hiyo kwenye viwanja vya Bunge mjini hapa jana, muda mfupi
baada ya Spika wa Bunge, Anna Makinda kusitisha shughuli za Bunge baada
ya kipindi cha maswali na majibu asubuhi, kutokana na wabunge wa
upinzani kugomea uwepo wa miswada hiyo katika orodha ya shughuli za
bunge za jana.
Lakini
akizungumzia kadhia hiyo, Rage alisema ina msukumo wa baadhi ya
wafanyabiashara wa mafuta, madini na gesi ambao hawataki miswada hiyo
iwasilishwe bungeni na kupitishwa kuwa sheria kwa sababu ina mambo mengi
yenye maslahi kwa nchi.
“Siku
zote tunapiga kelele tuone mikataba ya madini, gesi na mafuta tunataka
iwe wazi, leo Serikali inaleta bungeni sisi tunapinga, hapa kuna namna,
tunajua. Wapo baadhi ya wabunge wa upinzani na wengine hata wa CCM
wanatumika kwa maslahi ya wafanyabiashara. “Wapo baadhi ndani ya CCM
hawajui wanafuata mkumbo na baadhi wanatumika, lakini pia wapo wa
upinzani wanafuata mkumbo na wengine nao wanatumika, hili ni jambo kubwa
zaidi ya wengi wanavyofikiri,” alisema.
“Miswada
hii ikipitishwa na kuwa sheria itaweka uwazi katika leseni na mikataba
ya madini, gesi na mafuta, jambo ambalo ni jema, lakini kuna watu
hawataki jambo hili kwa maslahi yao binafsi, nawashauri wabunge
wasifuate mkumbo kwa mambo wasiyoyajua msukumo wake, kuna watu wanalipwa
kwa jambo hili,” alisema Rage.
Tundu
Lissu ashangaa Lakini akizungumzia tuhuma hizo katika viwanja vya Bunge
jana, Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, ambaye pia ni
Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) alisema jambo hilo
haliwezekani na ni kichekesho.
“Leo
kampuni za mafuta zinunue wabunge wa upinzani ambao hawazidi 100, halafu
iache wa CCM zaidi ya 260, maana nao hawautaki. Hakuna suala la
kutumika na wafanyabiashara, hapa ni suala la muda huu si mwafaka
kujadili miswaada hii. “Wabunge asilimia kubwa hatuitaki hii miswada,
isipokuwa nilichoambiwa ni kuwa serikali inapewa presha na wafadhili ili
iweze kupata fedha na kama wasipowasilisha bungeni miswaada hiyo
hawatazipata,” alisema Lissu.
Hata
hivyo, akizungumza na waandishi wa habari jana mchana kwenye viwanja
hivyo, Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene, alisema ni
kichekesho kutaka miswaada hiyo iahirishwe kwa kisingizo cha muda
hautoshi.
“Nawaambia
tusipopitisha sheria sasa itakuwa hasara kubwa kwa Watanzania, maana
wanasema tusubiri Bunge lijalo, lakini hatuna uhakika na uwezo wa
wabunge hao katika jambo hili, hivyo itabidi nao tuwajengee uwezo kama
wa Bunge la sasa. “Wabunge hawa wamejengewa uwezo wameenda nchi
mbalimbali kujifunza masuala ya gesi na mafuta na tangu mwaka 2010
tumeanza mchakato wa jambo hili, ndiyo sababu tunataka itungwe sasa
vinginevvyo itakuwa matatizo mbele,” alisema Simbachawene.
Alisema
hakuna msukumo wowote wa wafadhili ambao Serikali inaupata zaidi ya
maslahi ya Watanzania na kusisitiza kuwa masuala ya kujadili mikataba na
kampuni za gesi inachukua kati ya mwaka mmoja hadi mwaka mmoja na nusu,
hivyo kama sheria mpaka mwakani itakuwa haijatungwa na uzalishaji
umepangwa uwe kati ya mwaka 2018 na 2019 inamaanisha muda utazidi
kusonga mbele na itakuwa hasara kwa Watanzania.
“Suala la
majadiliano ya mkataba si la wiki moja au mwezi, ni kati ya mwaka mmoja
na zaidi, sasa unasema Bunge lijalo ndiyo lifanye kazi hiyo unajua
litakuwaje?
“Unasema
watu mawazo yao yapo majimboni, hapa tatizo ni uvivu na kutojiandaa kwa
baadhi ya wabunge majimboni ndiyo wanataka kuchangia miswaada
isiwasilishwe,” alisema, lakini akikataa kuzungumzia kama baadhi ya
wabunge wa upinzani wanatumiwa kukwamisha miswaada hiyo.
Pia
alisema miswaada hiyo sio mipya badala yake imepitia hatua zinazotakiwa,
ikiwa ni pamoja na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini
kuifanyia kazi na kuchukua maoni ya wabunge na wadau mbalimbali katika
kuiboresha na wamesaidia kwa kiasi kikubwa.
Alisema
pamoja na mambo mengine Muswada wa Sheria ya Uwazi na Uwajibikaji katika
Tasnia ya Uchimbaji ukipitishwa utafanya mikataba yote ya madini na
gesi iwe wazi na halitakuwa jambo la siri kama ilivyo sasa.
Pia
alisema ushiriki wa Watanzania lazima uwe wazi ijulikane wameshiriki kwa
kiasi gani tofauti na sasa na kwamba pia gharama za uwekezaji na
uzalishaji nazo zinatakiwa kuwa wazi, mambo ambayo ndiyo sababu wanataka
yaharakishe miswada hiyo.
Alisema
sheria italazimisha kujua taarifa kuhusu uwekezaji kama ni halisi na
sahihi na kwamba hilo ni jambo muhimu na ndiyo sababu wanataka uwazi uwe
katika sheria “Wanaoenda kufanya majadiliano ya kuingia mikataba sio
wabunge ni wataalam, ndiyo sababu tunataka kuwapa nguvu za kisheria,”
alisema Simbachawene. Imeandikwa na Amir Mhando na Namsembaeli Mduma.
(HABARI LEO)
Chapisha Maoni