Wanafunzi wanaodaiwa kutelekezwa na Staa anayevuna fedha nyingi kupitia kipaji chake cha muziki, Bongo, Nasibu Abdul ‘Diamond’.
Gladness Mallya
Chanzo makini kililiambia gazeti hili juzi kwamba, baada ya Diamond
kuwashindanisha watoto hao, Hillary na Hamis (katika picha no. 1 na 2
zilizoko ukurasa wa mbele walipelekwa shule na Diamond) katika shindano
la Ngololo lililonyika Januari, mwaka jana katika Viwanja vya Leaders
Club, Dar na kushinda aliamua kuwapeleka katika shule hiyo na kuahidi
kuwalipia ada kila mwaka lakini kuanzia hapo aliwatelekeza.
“Jamani Diamond kila kukicha anafanya shoo za mamilioni lakini
ameshindwa kuwalipia ada wale watoto ambao aliahidi kuwasomesha.
Wamesoma mwaka mmoja tu, mwezi uliopita walitimuliwa na sasa wako
nyumbani. Inauma sana kwani hawa watoto walitolewa kwenye shule za
kawaida na yeye ndiyo akawapeleka kule,” kilisema chanzo hicho.
WAZAZI WANASEMAJE?
Akizungumza na gazeti hili, mmoja wa wazazi wa wanafunzi hao, Fadhili
alisema watoto wao walitimuliwa shuleni tangu April mwaka huu kwa kuwa,
Diamond hakuwahi kuwalipia ada tangu alipowaingiza pale.“Inauma sana,
kwani tangu watoto wetu watimuliwe tumekuwa tukifuatilia kwa mtu
tuliyeambiwa ni msimamizi wa Diamond (jina lake linahifadhiwa kwa sasa)
lakini hatupi jibu la kueleweka.
“Tulipewa namba za simu za mameneja wa Diamond, Hamis Taletale ‘Babu
Tale’ na Said Fella lakini kila tukiwapigia simu tunaambiwa msanii huyo
hayupo Dar, mara amesafiri, mara yuko kwenye shoo, yaani kila siku
tunazunguka tu hatujui tufanye nini.
“Tunaomba sana jamani, mtusaidie na nyie waandishi maana watoto
wanapitwa na masomo na isitoshe kabla ya hapo walikuwa wakisoma kwenye
shule za kawaida,” alisema mzazi huyo.
MSIKIE MWALIMU MKUU
Paparazi wetu alifunga safari mpaka shuleni hapo maeneo ya Mikocheni,
Dar na kufanikiwa kuzungumza na Mwalimu Mkuu, Mercy Githirua ambapo
alithibitisha watoto hao kusimamishwa masomo kutokana na kukosa
ada.“Tulivumilia kwa muda mrefu sana kwani tulimwamini Diamond
tukawapokea watoto hao na kuanza masomo. Siku aliyokuja kuwakabidhi hapa
shuleni aliomba ‘invoice’ kwa ajili ya kututumia ada lakini yuko kimya
mpaka leo.
“Hata fedha ya kuwashonea sare za shule ilibidi niwasiliane na
(linatajwa jina, linasitiriwa) maana tunafanya naye kazi nyingi, akatoa
hizo fedha lakini ada ndiyo ikawa tatizo. Hivyo ilipofika Aprili 14,
mwaka huu ilibidi niwarudishe nyumbani mpaka kieleweke kwa kweli.
“Sijapenda tabia ya Diamond, hivi anajua watoto wakimchukia itakuwa ni
hatari sana kwake? Watoto wa watu walikuwa wanasoma huko akaenda kuwatoa
na kuwaleta hapa lakini amewatelekeza, siyo vizuri kabisa,” alisema
mwalimu mkuu huyo.
WANADAIWA SHILINGI NGAPI?
Kwa mujibu wa mwalimu mkuu huyo, watoto hao tangu walivyoingia Januari
21, 2014 hawakuwahi kulipiwa ada yoyote hivyo kila mmoja anadaiwa
shilingi milioni moja na laki sita (1,600,000).
DIAMOND, MAMENEJA WAKE!
Juzi, gazeti hili lilifanya jitihada za kumtafuta Diamond kwa njia ya
simu lakini ilikuwa imesetiwa kwamba inafanya kazi muda wote ‘bize’ hata
alipotumiwa meseji hakujibu. Vivyo hivyo kwa mameneja wake, Fella na
Bab Tale simu zao ziliita bila kupokelewa.
TUJIKUMBUSHE
Mwaka jana, Diamond aliandaa shindano la Nani Anaweza Kucheza Staili ya
Wimbo wa Ngololo ambapo watoto kibao walijitokeza Leaders Club. Watoto
hao wawili waliibuka kidedea kwa kuonesha uwezo mkubwa wa kucheza na
ndipo zawadi yao aliamua kuwapeleka kwenye shule hiyo na kukutwa na
yaliyowakuta!.
Credit:GPL
Chapisha Maoni