Nilichokisema jana kutokana na kauli ya Mhe. LOWASSA.
Mimi nilianza kushiriki siasa toka nikiwa mdogo sana. Kuanzia
Chipukizi, Greenguard wa UVCCM na baadaye UVCCM. Miaka ya mwanzo ya 90
nilivutiwa sana na mijadala ya mfumo wa vyama vingi ama kimoja.
Nakumbuka, binafsi nilivutiwa zaidi na mfumo wa kutanua demokrasia,
nakumbuka nilichangia hoja zangu kwenye mkutano wa tume pale Nzega
mjini, viwanja vya parking pembeni ya jukwaa. Wengi kwa hakika
hawakuunga mkono mfumo wa vyama vingi. Waliamini katika chama kimoja.
Nilijiunga rasmi CCM mwaka 1994. Mwaka 2005, niligombea Ubunge wa Jimbo
la Nzega, kura hazikutosha kwenye mchakato wa maoni ndani ya CCM na
vikao vilisema kuwa wakati wangu bado.
Niliendelea kufuatilia kwa ukaribu sana kilichokuwa kinaendelea
kwenye duru za siasa. Mijadala ya Bungeni ilikuwa ya moto sana, mara
nyingine ikitutia simanzi sisi vijana wa CCM haswa namna tulivyokuwa
tukishuhudia wabunge wachache sana wa upinzani wakiishambulia serikali
yetu ya CCM kuhusiana na wimbo mpya kwenye duru za siasa za miaka hiyo,
'ufisadi'. Ufisadi ikiwa ni order of the day. Ufisadi ikiwa ni mtaji na
ajenda kuu ya wapinzani Bungeni, of-course pia ajenda ya kikundi kidogo
cha wabunge wa CCM waliojitambulisha kama vinara wa kupinga ufisadi.
Miaka hiyo kila mtu akiuchukia ufisadi na mafisadi.
Mwaka 2008, mimi nikiwa kijana mwana mabadiliko na ninayechukia
ufisadi na mafisadi, kama walivyokuwa vijana wenzangu wengi, kwenye duru
za siasa na nje ya duru za siasa, nilivutiwa na mijadala iliyokuwa
Bungeni kutokana na hoja iliyowasilishwa bungeni na Dr. Harrison George Mwakyembe
kuhusiana na mchakato wa kununua umeme wa dharura, na zabuni hiyo
kupewa kampuni ya Richmond Development Company LLC ikidaiwa kuwa
mchakato huo ulikuwa na ubatilifu na mazingira ya rushwa ndani yake.
Nikiwa kama mwananchi mwenye strong affinity na siasa, uongozi na namna
nchi yetu inavyoendeshwa, nilivutiwa sana na namna wabunge wengi wa CCM
walivyoamka na kuonesha kwa dhati ya mioyo yao namna walivyokerwa na
ufisadi wa Richmond. Nakumbuka Mbunge wangu Lucas Selelii alikuwa kinara mmojawapo.
Mwanzoni sikutarajia kama Waziri Mkuu niliyempenda sana na kumuamini,
niliyemtazama kama kiongozi wa mfano kwangu, aliyenivutia sana kwa
namna alivyokuwa akichapa kazi na akitoa kauli za straight forward
kwenye mambo mengi ya msingi, akikemea uzembe, akiadhibu wabadhirifu
bila soni wala huruma, akifika kila kona ya nchi ambapo akitokea tu,
basi wazembe na wabadhirifu wanaangusha angusha karatasi hovyo, Mhe.
Edward Ngoyai Lowassa eti naye angehusishwa kwa namna yoyote ile!
Sikuamini. Lakini sikuamini zaidi niliposikia anajiuzulu...tena eti kwa
sababu ya Richmond.
Nakumbuka sana kwenye duru za siasa yeye na Mjomba wangu Mhe. Jakaya Kikwete
walipochukua fomu za kuwania Urais mwaka 1995, wakiwa na ujana ujana
mwingi na sisi tukiwashangilia na kuwapenda kama inspirational figures
wetu. Na ilipotokea mwaka 2005 alipoingia Mjomba, nilijua wazi kabisa
kuwa Waziri Mkuu angekuwa Mhe. Lowassa, na tulitabiri kipindi kile kuwa
Mhe. Lowassa angekuwa Rais baada ya kumaliza kipindi cha Uwaziri Mkuu,
yaani 2015. Nilisimamisha kagari kangu maeneo ya Biafra na kukimbia
kwenye Pub moja pale jirani kutazama televisheni iliyokuwa inarusha
kutoka Bungeni, nakumbuka watu walijaa kwa wingi sana na wengi
wakishangilia kuonesha kufurahishwa kwao namna serikali ilivyokuwa
ikiwajibika Bungeni. Sikuamini. Serikali imeanguka! Lowassa out.
Sikuamini kabisa.
Jana nikapata habari kuwa Mhe. Edward Lowassa amezungumza na wahariri
wa vyombo vya habari nchini - amekana kuhusika kwake na Richmond.
Nikashtushwa sana na hili. Nikajiuliza hivi ni nini kinataka kutokea
kwenye siasa za nchi yangu? Mjadala wa Richmond ulifungwa Bungeni miaka 7
iliyopita, je inabidi ufunguliwe upya, na watu wapya tutafakari upya?
Maana kuna minong'ono kuwa Mhe. Lowassa anataka kuwania Urais mwaka
2015, na ana mpango wa kutangaza nia muda si mrefu. Nikajiuliza, ni kwa
nini imemchukua Mhe. Lowassa zaidi ya miaka saba kujibu hadharani kuwa
hakuhusika na Richmond? Kwa nini anatamka maneno haya leo na kwa nini
hakujitetea Bungeni siku ile alipojiuzulu? Nakumbuka siku ile alisema
tatizo ni uWaziri Mkuu, kwa nini hakufafanua na alikuwa na fursa hiyo
kama 'primus inter pares (first among equals)?' Kipindi fulani
alisemekana kuwa ni 'gamba' na lingepaswa kuvuliwa...likaishia kiunoni!
Ni kwa nini halikuvuka? Maswali haya sijawahi kuyapatia majibu.
Hivi ilikuwaje Rais wa Nchi, ambaye ni Mwenyekiti wa CCM, Kamati ya
Wabunge Wote wa CCM Bungeni, na mamlaka zote za kiserikali kushindwa
kumlinda Waziri Mkuu wake dhidi ya tuhuma za kuhusika kwake kwenye
Richmond mwaka 2008? Maana kwenye siasa za mabunge yanayofuata mfumo wa
Westminster, Waziri Mkuu ni 'primus inter pares', kwamba ana fursa ya
kwanza ya kuzungumza kwenye mijadala Bungeni na ana-enjoy nguvu ya kuwa
na majority bungeni kuendesha mambo ya serikali na kutawala mijadala na
maamuzi. Ilikuwaje Chama kilimuacha Waziri Mkuu wake akaanguka?
Ilikuwaje? Maswali: je kulikuwa na ukweli dhidi yake kuhusiana na tuhuma
za Kamati? Ama Kamati ilitumika vibaya na mahasimu wake? Yeye amekana,
sasa wanakamati inabidi wamjibu watuweke wazi, na wamjibu kwa uwazi bila
kuficha, maana kama alionewa ijulikane na sisi tuliohuzunishwa ama
kufurahishwa na Bunge wakati ule tuujue ukweli. Yeye anasema hakuhusika
na ndiyo maana Kamati ya Mwakyembe haikuona haja ya kumwita kumhoji.
Ukweli tunauhitaji sana leo kuliko jana. Ukweli huu ni haki yetu.
Kama Kamati ilimuonea, basi imuombe radhi na ituombe radhi watanzania wote. Kama kweli Mhe. Lowassa atagombea Urais Twentyfifteen,
itakuwaje kwenye mijadala ya uchaguzi na CCM itasimamaje (kama
itampitisha kuwa mgombea) kumuombea kura wakati ilimuangusha Bungeni
kutoka kwenye nafasi nyeti ya Uwaziri Mkuu? CCM itatoa majibu gani
kuhusu kwa nini ilimuita 'gamba' na ikatangaza hadharani kuanza mchakato
wa kuvua magamba (ambao haukukamilika). Nilisema jana, Mhe. Lowassa
amefungua pandora box, na kama atatangaza kweli kuwania Urais, inabidi
haya mambo yawekwe wazi, yamalizwe, maana hauwezi jua ya kesho -
ikitokea akawa mgombea wetu, tutaanzia wapi kumnadi na kusema ni mtu
safi, muadilifu, anayechukia rushwa na ubadhirifu na kwamba anafaa kuwa
Rais, wakati juzi tulisema hafai kuwa Waziri Mkuu na tukamtoa? Nilisema
jana kuwa , CCM haipaswi ku-risk kuteua wagombea wenye mambo mengi ya
kutolea maelezo kwa wananchi, ikifanya hivyo itaangushwa asubuhi ya saa
nne. Watanzania wa leo siyo wa juzi.
Chapisha Maoni