0
Aidha, Kikwete amewaaga mabalozi na kuipongeza wizara ya mambo ya nje kwa kusema kuwa katika utawala wake, ndio wizara ambayo haijamsumbua. Akizungumza katika mkutano wa nne wa mabalozi wa Tanzania katika nchi za nje, uliofanyika jijini Dar es Salaam jana, Rais Kikwete aliwataka kutotetea Watanzania wanaofanya uhalifu, ikiwemo kukamatwa na dawa za kulevya, ubakaji isipokuwa, kama upo uonevu.
Rais ajaye Kikwete alisema kazi kubwa ni kujenga uhusiano mzuri na nchi zingine, hivyo kuwa na marafiki zaidi ya maadui.
“Mwalimu (Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere) kuna mambo aliniambia wakati akisuluhisha mgogoro wa Burundi, kuwa jambo jema ni kujenga urafiki na nchi zingine ambao wanaweza kukusemea vizuri mambo yako, lako linakuwa lao. “Mimi nimeingia madarakani nimeikuta nchi ikiwa haina adui na nimeiacha nchi ikiwa haina adui, hivyo ni vema kuendeleza hili na kutokuwa mchokozi,” alisema.
Wizara sikivu

Aidha, Kikwete alisema wizara ya mambo ya nje na watendaji wake, wamekuwa ni msaada mkubwa katika mafanikio ya nchi na imekuwa haimsumbui, tofauti na baadhi ya wizara (hakuzitaja), ambazo alilazimika kuingilia kati ili mambo yaende.
Wahalifu nje

Rais alisisitiza kwamba serikali haitawatetea watanzania watakaofanya uhalifu nchi za nje, ikiwamo wale wanaofanya biashara ya dawa za kulevya.
“Kama hapa tunawakamata wanaofanya biashara ya dawa za kulevya anapewa ‘mvua’ 30, au kibaka anafungwa miaka 30 au maisha, sasa kwa nini watu wetu wakifanya uhalifu huo watetewe, msiwatetee. Siyo kazi yenu, ila wanaoonewa wateteeni,” alisema.

Aliwataka mabalozi kuhakikisha wanajifunza na kuelewa mitandao ya uhalifu wa kimataifa, ugaidi, biashara ya dawa za kulevya na ujangili ili kujua jinsi vita ilivyo kubwa na jinsi ya kunusuru nchi, kwani haiko salama.
“Miaka ya nyuma mambo ya ugaidi tulikuwa tunasikia nchi za nje, tena za mbali, lakini sasa majirani zetu wanakumbwa na matatizo hayo, hata hapa nchini tumekumbwa na matukio ya hapa na pale,” alisema.

Aliongeza: “Hata ujangili nalo ni tatizo kubwa na ndiyo maana kuna pembe za ndovu zilipitia bandari ya Mombasa, zilipopimwa zilionesha ni tembo wa Ruaha na Selous, lakini zingine zilipitia Bandari ya Dar es Salaam lakini ni za tembo wa pinki wa Afrika ya Kati, hivyo ni vyema mkajua mtandao, washiriki ili kuisaidia nchi katika uhalifu huo.”
Masoko, biashara
Aidha, Rais Kikwete aliwataka mabalozi kuhakikisha wanatumia uwakilishi wao katika kutengeneza fursa za biashara na masoko, kusaidia kuinua uchumi na kupunguza umasikini kwa Watanzania na kufikia dira ya taifa ya maendeleo ya mwaka 2025.

“Msiishie kuhudhuria hafla, nitafarijika sana kama katika ripoti zenu mtakuwa mkielezea na fursa ambazo Watanzania watachangamkia, kama Misri wanataka vipapatio, mnaeleza ili Watanzania wafuge kuku wengi, wale kuku na vipapatio,” alisisitiza.

Alisema serikali imefanya jitihada kubwa za kuinua uchumi wa nchi kwa kushughulikia changamoto zinazozuia ukuaji wa uchumi, kama vile miundombinu ya barabara na umeme.
Alieleza kwamba kwa sasa asilimia 36 ya Watanzania, wanapata umeme wakati awali ilikuwa asilimia 10. Kwa mujibu wa rais, Agosti mwaka huu utaanza ujenzi wa reli mpya.
Alisema juhudi za sasa ni kuinua kilimo kinachojumuisha watanzania ili kupunguza umasikini.

Waziri Membe
Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, alisema mkutano huo wa nne wa mabalozi, unatoa fursa kwa wanadiplomasia hao kujifunza mambo mbalimbali ya maendeleo ya uchumi, mwelekeo wa uchumi, changamoto za ulinzi na usalama na utawala bora.

Mabalozi wamuaga
Naibu Mlezi wa Mabalozi, Balozi John Kijazi, alimpongeza Rais Kikwete kwa uongozi wenye mafanikio. Alimwombea heri katika kusimamia mchakato muhimu wa upatikanaji wa serikali mpya.

Chapisha Maoni

 
Top