
WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amezungumzia kwa mara ya kwanza sakata la Richmond lililosababisha ajiuzulu wadhifa huo, akisema alichukua tahadhari katika suala hilo na kuwa ubishi wa kisiasa umeligharimu Taifa kulipa mabilioni ya dola za Marekani.
Mbali na hilo, Lowassa anayejipanga kuwania urais kupitia CCM, ametaka watu waache kumchonganisha na Rais Jakaya Kikwete, huku akimsifu kwa kutekeleza kwa mafanikio Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
Aidha, amesema hana mpango wa kukihama Chama Cha Mapinduzi (CCM), na pia ametoa changamoto kwa wanaCCM wanaotaka kuwania urais wapimwe afya zao.
Lowassa aliyasema hayo jana katika mkutano wake na wahariri wa nyombo mbalimbali vya habari nchini uliofanyika nyumbani kwake Area C mjini hapa.
Lowassa aliyejiuzulu wadhifa wake huo Februari 2008, akihusishwa na sakata la Richmond – kampuni ya kufua umeme iliyoletwa nchini mwaka 2006 baada ya kuwapo kwa matatizo makubwa ya nishati ya umeme, alitoa sababu nne za kukaa kimya tangu wakati huo.
Alizitaja kuwa kwa mwanasiasa kukaa kimya pia ni silaha, hivyo aliamua kukaa kimya; kuogopa upotoshaji wa vyombo vya habari, siasa kuwa za uhasama, kusingiziana na kuogopa kuanzisha malumbano zaidi katika jamii.
Kuhusu Richmond alisema ‘zengwe’ hilo limeeleweka nchini kwani limeandikwa sana na kuzungumzwa sana.
“Kama alivyoeleza Mheshimiwa Mbowe bungeni hivi karibuni, ubishi ule umegharimu bilioni 120 (Dola za Marekani), tulitaka kuvunja mkataba wa Richmond. “Nikasema wataalamu wasituingize mkenge, nikamwita Mwanasheria Mkuu wa Serikali nikamwambia kuna story hii, be careful. (Anasema iliandikwa na gazeti la The Guardian).
Kuhusu uhusiano wake na Rais Kikwete, Lowassa ambaye alisema Jumamosi atatangaza nia yake ya kuwania urais akiwa Arusha, aliwataka watu waache kumchonganisha na mkuu huyo wa nchi.
“Kwa nini urafiki wetu uwe ajenda? Kwa nini mnapandikiza hilo, yeye ni rafiki yangu, acheni maneno yasiyo na maana,” alisema Lowassa na kuongeza kuwa hata kama walichukua fomu pamoja mwaka 1995, lakini miaka mingi imepita na muhimu ni kuangalia kama urafiki wao umeshawishi kitu fulani.
Akizungumzia utajiri wake, mwanasiasa huyo alikiri kumiliki nyumba kadhaa (hakuzitaja idadi) na pia anazo ng’ombe kati ya 800 hadi 1,000, lakini akaongeza kuwa anauchukia umasikini na anatamani utajiri. “Hili ni swali zuri sana, lakini mtashangaa majibu yangu.
Namiliki nyumba kadhaa na nina ng’ombe kati ya 800 na 1,000. Na kule kwetu ninakotoka, ili uwe kiongozi lazima uwe na mifugo ya kutosha,” alisema na kuongeza: “Lakini kama watu wanataka kufahamu utajiri wangu waende Sekretarieti ya Maadili, unalipa kidogo utasoma kila kitu. Lakini ngoja niseme kidogo, natamani utajiri.
“Tuache kuwabeza matajiri, tuache kukumbatia umasikini. Kuwa na matajiri kama Mzee Mengi, Bakhresa, kina Karamagi, ni jambo zuri sana na hawa ni role model, tungekuwa nao 20,000. “I hate (nachukia) umasikini. Nataka uongozi ili kuwaondoa Watanzania katika umasikini. Kama mtu amepata utajiri kwa njia za uhalali, amejinyima, ni nzuri sana.
Nachukia watu wanaopata fedha na kuishia katika ulevi na wanawake. Kina mama mnisamehe. Sitaki kupata uongozi kwa kudanganya, nachukia umasikini.” Alipoulizwa kuhusu harambee mbalimbali anazozifanya misikitini, makanisani na kwingineko na kuchangia mamilioni ya fedha, Lowassa alizitetea harambee hizo na kueleza kuwa fedha zinachangwa na marafiki zake.
“Zile sio fedha zangu, kwa mfano kule Arusha juzi, zilichangwa milioni 200, watu wamesema nimechangia Shilingi milioni 200, hapana. Mimi na marafiki zangu wa Arusha, Dar na kwingineko tumechanga Shilingi milioni 100, Makamu wa Rais amechangia Shilingi milioni 10,” alieleza Lowassa na kuongeza: “Kuchangia misikitini, makanisani na katika maendeleo ni jambo zuri, kwa wenzetu wa Kenya harambee ndio kila kitu. Nawashauri viongozi na wabunge kwenda vijijini kusaidia maendeleo kwa njia ya harambee.
“Hili la shule za kata ambalo ni mawazo ya CCM na maelekezo ya Rais, limefanikiwa kwa nguvu za Serikali na wananchi, kwa hiyo harambee zinafaa.”
Kuhusu afya yake, alisema yuko fiti na ni upuuzi kusema kuwa ni mgonjwa, na akatoa changamoto kwa wanaCCM watakaojitokeza kuwania urais, wakapimwe afya zao.
“Nimetembea pale Dar kilometa tano, wakasema siwezi kukimbia hata meta 100 na kuwa nimepelekwa Ujerumani kutibiwa. Huu ni upuuzi, ni chuki kutakiana mabaya. Niko fit and kicking. Fit kwa chochote kile. “Tukapimwe afya zetu kujua nani mgonjwa, tutakutana kwenye uwanja wa mapambano, na I will beat them by far (nitawashinda kwa mbali).”
Alipoulizwa kama asipoteuliwa na CCM kuwania urais, atahama chama hicho, tawala, Lowassa alisema hana mpango B katika hilo, na CCM ni haki yake.
“Sina mpango wa kuhama. Nimeingia CCM mwaka 1977 na sijawahi kutoka katika majukumu yake zaidi ya pale nilipokuwa Mkurugenzi Mtendaji wa AICC. “My right is CCM (haki yangu ni CCM), sio kwa hao kina kadeti. Huyo ambaye hanitaki CCM ndio ahame. Hakuna mpango B, nina mpango A na naamini utafanya kazi,” alisema Lowassa ambaye aliwania urais wa Tanzania mwaka 1995.
Aidha, akizungumzia kuhusu madai kuwa akiwa Rais atalipiza kisasi, Lowassa alisema yeye ni Mkristo, na imani yake inamtaka kusamehe mara 70, hivyo hatalipa kisasi, moyo wake ni mweupe na yaliyopita yamepita.
Akitoa maoni baada ya kuulizwa kuhusu chama chao CCM, Lowassa alisema chama hakitakiwi kubweteka kwani upinzani umepata nguvu sana mijini na vijijini.
“Tusibweteke wenzetu wamejiandaa, na mkiondolewa hamrudi madarakani, angalia KANU, UNIP na vinginevyo. Lakini faida kubwa ya CCM ni kuwa Rais Kikwete ametekeleza vizuri sana Ilani, hii ndio kete yetu, jamaa mmoja alisema mtaji wetu, lakini isitubweteshe, tutatue matatizo ya wananchi na watu wahimizwe kujiandikisha kwa wingi,” alibainisha mwanasiasa huyo.
Lowassa ambaye baadhi ya maswali aliyajibu juu juu au kukataa kuyajibu kwa kuwa alisema yapo katika hotuba yake ya Jumamosi mkoani Arusha, alisisitiza suala la elimu kuwa kipaumbele namba moja na pia tatizo la ajira kama bomu lisiposhughulikiwa ipasavyo.
Lowassa alipoulizwa kama angekuwapo serikalini hadi sasa na akaomba kuwania urais, alisema: “Naamini kwa kasi ile, ningepunga mkono, na kuzoa kura zote. Lakini nasikitika hatufanyi maamuzi, yawe mabaya au mazuri. Rais amefanya kazi nzuri, lakini hatukupaswa kuachwa nyuma na Waganda, Wanyarwanda.”
Chapisha Maoni