
Mh. Edward Lowassa.

Mh. Bernard Membe.

Mh. Stephen Wasira.(KILONGE)

Mh. January Makamba.

Mh. William Ngeleja

Mh. Fredrick Sumaye.
Dodoma. Mpambano
mkali wa kuwania nafasi ya kuteuliwa kugombea urais kwa tiketi ya CCM
sasa umeanza rasmi baada ya Kamati Kuu ya chama hicho tawala kuwaweka
huru makada sita waliokuwa wamefungiwa kwa takriban miezi 17 kwa makosa
ya kukiuka kanuni za uchaguzi.
Kufunguliwa
kwa makada hao, ambao baadhi yao wanapewa nafasi kubwa ya kupitishwa na
chama hicho, kumekuja wakati CCM ikikabiliwa na tishio la kutokea
mgawanyiko mkubwa, hasa kutokana na baadhi ya kambi kuituhumu
sekretarieti kuwa inabagua baadhi ya wagombea.
Makada
waliofungiwa tangu Februari, 2014 kwa kosa la kuanza kampeni mapema ni
mawaziri wakuu wa zamani, Frederick Sumaye na Edward Lowassa, ambaye kwa
sasa ni mbunge wa Monduli.
Wengine
ni Bernard Membe, ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Steven Wasira (Waziri wa Kilimo na Chakula), January Makamba
(Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia), na mbunge wa Sengerema, William
Ngeleja.
Baadhi ya
wanachama wa CCM, hasa wajumbe wa Halmashauri Kuu, walianza kumiminika
nyumbani kwa makada hao mara baada ya kupata taarifa za kuondolewa kwa
adhabu hiyo, wengi wakionekana kwenda kumpongeza Lowassa.
Kufunguliwa
kwa makada hao ni mwanzo wa kinyang’anyiro kikali cha kuwania kumrithi
Jakaya Mrisho Kikwete kwenye nafasi ya urais na mwenyekiti wa chama
hicho kikongwe na dalili zote za kuwapo kwa vita kali zilianza mara moja
jana baada ya kutangazwa kwa uamuzi huo.
Makamba: Safari ya ushindi
“Nimefurahishwa
na uamuzi wa Kamati Kuu. Safari ya ushindi sasa inaanza,” alisema
Makamba alipohojiwa kuhusu tamko hilo la Kamati Kuu.
“Sijashangaa
hata kidogo (kusikia uamuzi huo) kwa kuwa sijawahi kukiuka maadili ya
chama. Sasa nasubiri muda wa kampeni kutangazwa ili nianze kufanya hivyo
kwa kuzingatia kanuni za chama kwa sababu najua wakati wa mchujo wa
wagombea, CCM itaangalia tena jambo hili.”
Ngeleja: Nasubiri muda
Ngeleja,
ambaye alikuwa Waziri wa Nishati na Madini, aliishukuru Kamati Kuu kwa
kufikia uamuzi huo akisema imezingatia misingi yote ya haki na kwamba
kilichobaki ni kusubiri muda wa kampeni.
“Hatua
inayofuata ni kuhakikisha kwamba nafuata kanuni, taratibu na miongozo ya
chama katika kugombea nafasi nitakayoiomba,” alisema mbunge huyo wa
Sengerema.CHANZO NA MWANANCHI
Chapisha Maoni