Kiongozi
wa ofisi na mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi
na Utamaduni (UNESCO) nchini, Zulmira Rodrigues (kulia), akielezea nia
ya Shirika lake kusaidia mapambano dhidi ya unyanyasaji na dhuluma
zinazofanywa jamii dhidi ya watu wenye albinism nchini alipomtembelea
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo ofisini kwake jijini Mwanza.
SHIRIKA
la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) limeahidi
kusaidia mapambano dhidi ya unyanyasaji na dhuluma zinazofanywa jamii
dhidi ya watu wenye albinism.
Kauli
hiyo imetolewa hivi karibuni na Kiongozi wa ofisi na mwakilishi wa
Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO)
nchini, Zulmira Rodrigues wakati akizungumza na mkuu wa mkoa wa Mwanza
Magesa Mulongo.
Mwakilishi
huyo wa Unesco amesema hayo alipomtembelea Mkuu wa mkoa kumsalimia na
kumweleza hatua zinazochukuliwana Unesco katika kukabiliana na ukatili
dhidi ya watu wenye albinism.
Akifafanua
zaidi alisema kwamba UNESCO haijatenga fedha zitakazotumika kuendesha
kampeni mahsusi bali itatumia uwezo wa kiufundi uliopo kwa wataalamu
walionao na kwamba wanakusudia kuona kwamba miaka 15 ijayo watoto
wanaozaliwa nchini Tanzania wanakuwa huru pasipo na viashiria vya
kuhatarisha maisha vinavyosababishwa na mauaji ya watu wenye albinism.
Akimkaribisha
Bi Zulmira ofisini kwake, Mkuu wa mkoa Magesa Mulongo alisema kwamba
ingawa kuna utulivu katika kipindi hiki mkoani Mwanza, bado mkoa wake
unaendelea kukabiliana na viashiria vinavyosababisha ukatili kwa watu
wenye albinism na wazee.
Bwana
Magesa alisema imani potofu zilizopo zinazosadikika kufanikisha biashara
za uvuvi wa samaki, uchimbaji wa madini na wanasiasa kuendelea na
madaraka ni miongoni mwa sababu kubwa za mauaji hayo yaliyoitia doa
jeusi jamii ya kitanzania nje ya mipaka.
Alisema
kwamba jitihada zinafanywa kukabiliana na imani hizo potofu kwa
kuihamasisha jamii kutoziamini na kwamba madaraka na utajiri unatokana
na juhudi, kufanya kazi kwa bidii na si vinginevyo.
Aidha
amesema mkoa wake umekuwa ukihakikisha kwamba makundi yanayotumika kuua
watu wengine kwa kushirikisha jamii yanavunjwa na pia kuwachukulia hatua
kali wote wanaobainika kushiriki kwa njia moja au nyingine.
Hata
hivyo mwakilishi wa umoja wa mataifa alisema kwamba hali ya amani
itatawala pale tu watu watakapobaini kwamba kuua ni ukiukwaji wa haki za
binadamu na ni kosa la jinai.
Alisema
pindi binadamu watakapokiri kwamba binadamu wote ni sawa na kuishi na
albinism sio 'mzimu' watabadili mwelekeo mzima wa fikra potofu kimaisha
na kuishi kwa amani na kuthaminiana.
Bi
Zulmira alimwambia mkuu wa mkoa kwamba UNESCO kwa kushirikiana na wadau
wengine wataendesha makongamano yenye lengo la kushirikisha jamii katika
kuandaa na kutekeleza mikakati itakayo changia kuzuia na kutokomeza
unyanyasaji na dhuluma zinazofanya dhidi ya watu wenye albinism.(Muro)
Chapisha Maoni