Marehemu Sarah enzi za uhai wake.
Stori: Waandishi Wetu
“KWA kweli sisi kwetu kama kanisa ni maajabu na mshtuko. Inapotokea
ajali kama hii bila kutarajia lazima kutokee mshtuko. Hakuna anayependa
kutokea kwa hali hii, tumuombe Mungu. Najua mengi yatasemwa lakini
ukweli ni kumuachia Mungu tu,” ndivyo alivyoanza kusema Askofu Yekonia
Byabaza ambaye ni Msaidizi wa Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima,
Josephat Gwajima.
Askofu Byabaza aliyasema hayo alipozungumza na Gazeti la Uwazi kufuatia
vifo vya watoto wawili ndugu wa damu moja, Sarah (10) na Goodluck David
Oturo (4) waliokufa kwa kunaswa na umeme wakiwa kwenye ibada katika
kanisa hilo, Kawe jijini Dar wiki moja iliyopita.
Askofu huyo alizungumza na Uwazi kwenye ibada maalum ya kuaga miili ya
marehemu hao iliyofanyika nyumbani kwa wazazi, Mbezi Juu jijini Dar es
Salaam, Alhamisi iliyopita.
Aliendelea kusema: “Ninachokijua ni kwamba hali hiyo imetokea kwa wote
baada ya Goodluck ambaye ni mdogo alipoona dada yake amenaswa na umeme
alimfuata na kumgusa huku akilia na kusema; dada… dada…ndipo na yeye
akanaswa lakini siyo kwamba kuna jambo. Mungu alipanga kuwa vifo vyao
vitatokana na njia hiyo.”
Marehemu Goodluck enzi za uhai wake.
MASWALI YA WANAFUNZI
Katika msiba huo uliowaacha midomo wazi waombolezaji, wanafunzi waliokuwa wakisoma na Sarah walikuwa na maswali kwa muda mrefu:
“Kwa nini iwe familia hiyo tu? Kwa nini iwe Sarah na mdogo wake tu?
Mbona kulikuwa na watoto wengi! Halafu tunasikia waya uliomnasa Sarah
haukuwa umechubuka, sasa kwa nini anaswe?”
Wanafunzi hao muda mwingi walikuwa wakitokwa machozi kupindukia huku wengine wakiishiwa nguvu.
Mmoja wa wanafunzi aliyejitambulisha kwa jina moja la Samuel alisema
kwamba, Sarah alikuwa mpole na alikuwa akipatana na kila mmoja, hakuwa
mgomvi na alikuwa ana uwezo mkubwa darasani.
KITAALAM
Mtu mmoja msibani hapo ambaye alijitambulisha kuwa ni fundi umeme,
alisema kuwa, kwa umeme wa majumbani, mtu akivaa viatu hata kama
atakanyaga waya wenye umeme si rahisi kunaswa na kufa.
“Napata shida sana kama kweli Sarah alikanyaga waya wenye umeme. Mbona
alivaa viatu tena viatu vyenyewe havikuwa na chuma, kwa nini anaswe?
Haya kwangu ni maajabu hasa ninapoambiwa hata huo waya wenyewe haukuwa
umechubuka,” alisema fundi huyo.
MAJIRANI, WAALIMU WAZIMIA
Ili kuonesha kuwa, vifo vya watoto hao viligusa wengi, baadhi ya
majirani sambamba na walimu wa marehemu Sarah, jumla yao ikipata tisa,
walianguka na kupoteza fahamu wakati wakipita kwenye majeneza kuiaga
miili hiyo.
Baba wa marehemu hao(katikati) akiaga miili ya wapendwa wake.
MSEMAJI WA FAMILIA
Kutokana na hofu na mkanganyiko wa vifo hivyo kutanda, gazeti hili
lilizungumza na ndugu wa karibu wa marehemu hao ambaye hakupenda jina
lake liandikwe gazetini na kumuuliza juu ya maoni ya familia hiyo ambapo
alikuwa na haya ya kusema:
“Kwa kweli kwangu haya ni maajabu! Mimi si msemaji mkuu wa familia
lakini ninachokijua ni kwamba, marehemu kabla ya vifo vyao
walishatuhangaisha sana kwa kuumwa, hasa Goodluck. Na ajabu ni kwamba,
kuumwa huko, tulipowapeleka hospitali hawakupata nafuu lakini
tulipowapeleka kwa waganga wa kienyeji walipona.
“Kifupi ni kwamba, ukisimuliwa historia ya maisha yao kwa ujumla
ilitafsiri vifo. Inatuuma sana! Ajabu ya magonjwa yao, walikuwa
wakipelekwa kwa waganga wa kienyeji wanapata nafuu.“Baba yao amehangaika
nao mpaka basi hali iliyomfanya mama yao kuamua kuwapeleka katika
maombi kwa Askofu Gwajima.”
Msemaji huyo: “Nakumbuka Goodluck akiwa na umri wa miaka miwili, siku
moja tukiwa ndani ya nyumba iliibuka harufu ya dawa za kienyeji, ghafla
yeye alianza kunyooka huku akipoteza fahamu. Alipelekwa hospitali
ikashindikana, akapelekwa kwa waganga wa miti shamba akapata nafuu.”
MWAKA MMOJA BAADAYE
“Baada ya mwaka moja alianza kuumwa tena, akawa anatembea huku
akizunguka huku na kule bila kusema na mtu. Alionekana kama yupo kwenye
ulimwengu wa pekee. Aliweza kupona kwa mganga.
“Safari ya tatu akawa anatembelea makalio huku Sarah naye akianza kuumwa
tumbo na kuwa mpole sana. Tuliamua kuwapeleka hospitali mbalimbali
lakini hawakupona, tulipowapeleka kwa mganga wa miti shamba wakapona.
“Ndipo tulipogundua kuwa kuna mchezo mchafu unafanyika na hapo ndipo
mama yao akawa anakwenda nao katika maombi. Nafikiri mengi zaidi
mkamuulize baba yao.”
WAZAZI WASIMULIA
Baba mzazi wa marehemu hao, David Oturo yeye kwa upande wake alikiri
kuumwa kwa watoto hao magonjwa ya ajabu ambapo alipokuwa akiwapeleka
hospitali hawakupona bali walipata nafuu walipopewa dawa za kienyeji.“Na
mimi nimepatwa na mshtuko kuhusiana na vifo vya watoto wangu.
Nimehangaika nao kwa muda mrefu na nilijua wameshapona, ndiyo maana
nilimruhusu mama yao kwenda nao kwenye maombi. Sikutegemea kama mauti
yangewakuta wote kwa siku moja kule kanisani. Lakini yote namuachia
Mungu,” alisema kwa masikitiko mzazi huyo.
Akizungumza na Uwazi, mama mzazi wa marehemu hao alisema:
“Vifo vya watoto wangu siku hiyo kama niliviona tangu nyumbani. Ajabu ni
kwamba, moyo wangu siku hiyo ulikuwa na ganzi kwenda kanisani. Lakini
nikajipa nguvu tukaenda, kumbe ningeusikiliza moyo nikaacha kwenda,
wanangu wasingekufa.
“Lengo la kuwapeleka kwa Askofu Gwajima ni kuombewa ili magonjwa ya
ajabuajabu yawatoke, wawe salama nikijua hata kukwepesha vifo vyao maana
kusema ule ukweli mimi na mume wangu tulihangaika nao sana, nikajua kwa
Gwajima ndiyo nimefika kumbe bado!
Majeneza yaliyobeba miili hiyo yakiombewa kwa ajili ya mazishi.
MIILI YASAFIRISHWA
Miili ya watoto hao ilisafirishwa Ijumaa iliyopita kwenda Musoma mkoani
Mara kwa mazishi yaliyofanyika Jumamosi. Oturo kwa sasa amebaki na mtoto
mmoja wa kiume, mkubwa kwa wote.
Uwazi linatoa pole kwa familia ya Oturo kwa msiba mkubwa uliowapata na
Mungu awape uvumilivu. Bwana ametoa Bwana ametwaa, jina lake lihimidiwe!
Amina.Imeandaliwa
Na: Makongoro Oging’, Shani Ramadhani, Haruni Sanchawa na Gabriel Ng’osha.
Credit:GPL
Chapisha Maoni