UWEZEKANO
wa kufanyika kwa Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa kabla ya
Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, umeanza kupungua na kusababisha Kamati Kuu
(CCM) ya Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM, kuagiza Serikali na Tume ya Taifa
ya Uchaguzi (NEC), kutafakari upya kura hiyo.
Katibu wa
NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alisema hayo jana alipozungumza na
waandishi wa habari kuhusu kikao cha CC ya chama hicho kilichofanyika
kuanzia juzi asubuhi mpaka zaidi ya saa sita za usiku.
Kwa
mujibu wa Nape, CC ilipokea taarifa kuhusu mwenendo wa Kura ya Maoni na
baada ya kuitafakari kwa kina na kwa kuzingatia changamoto zilizopo
ikiwemo ya Uchaguzi Mkuu mwaka huu, wameona watoe ushauri huo.
Akielezea
changamoto walizoziona, Nape alisema wamebaini moja ni kasi ndogo ya
uboreshwaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura, ambalo hata NEC
imeshasema kuwa, Kura ya Maoni haitafanyika bila kukamilika kwa daftari
hilo.
Changamoto
ya pili ameielezea kuwa ni matakwa ya kisheria, ambayo ni kuwa na siku
60 za kutoa elimu ya Katiba Inayopendekezwa na siku 30 za kampeni,
ambapo inaonekana wanaweza kujikuta wamefikia Uchaguzi Mkuu kabla kura
hiyo haijafanyika.
"Tunadhani
ni wakati muhimu Serikali ikae na NEC ambao ni wadau kisheria wa suala
hili, kujadiliana kuona wanaliwekaje suala hili, kama ni kuhitimisha au
watafanyaje lakini kwa kuzingatia maslahi mapana ya Taifa letu," alisema
Nape.
Akifafanua
zaidi alisema pia ipo changamoto ya Uchaguzi Mkuu wenyewe, ambao Taifa
linaukaribia ambao Kikatiba ni Jumapili ya mwisho ya Oktoba, itakayokuwa
tarehe 25.
Nape
alisema baada ya kuhesabu siku zilizobakia kabla ya kufikia siku ya
Uchaguzi Mkuu, wamebaini kutakuwa na changamoto ambazo wameona
zinatakiwa kufanyiwa kazi, ili kutoa muda kwa Uchaguzi Mkuu ufanyike
kwanza bila kuingiliwa na mambo mengine.
Akizungumzia
uwezekano wa kufanya uchaguzi pamoja na Kura ya Maoni, Nape alisema
sheria haizuii lakini aliwahi kuhudhuria kikao kimoja cha Tume, baada ya
mjadala walikubaliana kuwa suala hilo haliwezekani.
Alifafanua kuwa hawawezi kuruhusu Katiba ivunjwe kwa kushindwa kufanya uchaguzi kwa muda unaopangwa kutokana na Kura ya Maoni.(HABARI LEO)
Chapisha Maoni