WAZIRI wa
Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi amesema vijana wote
waliohitimu kidato cha sita mwaka 2013/14, 2014/15 na kutojiunga na
mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) bila ridhaa ya jeshi hilo,
wanaendelea kusakwa na kuorodheshwa kwenye orodha ya watoro na upo
uwezekano wa wao kwenda mafunzo hayo mapema mwezi ujao.
Akiwasilisha
hotuba ya wizara hiyo bungeni jana ya Makadiro ya Mapato na Matumizi ya
fedha kwa mwaka 2015/16, Dk Mwinyi alisema mafunzo ya JKT kwa wahitimu
hao hutolewa kwa mujibu wa Sheria, ambapo ni ya kuwajengea uzalendo,
ukakamavu, maadili mema, utaifa na kutoa stadi za kazi.
Alisema
kwa mwaka 2014/15 jumla ya vijana waliopata mafunzo hayo kwa mujibu wa
sheria ni 31,635 ambayo ni sawa na ongezeko la vijana 15,632,
ukilinganisha na vijana 16,003 waliohitimu mafunzo hayo mwaka 2013/14 .
"Hata
hivyo idadi hiyo ni pungufu ikilinganishwa na idadi ya vijana 41,000
waliohitimu kidato cha sita, waliostahili kujiunga na mafunzo hayo, na
sababu zilizofanya upungufu huo ni pamoja na kalenda ya awamu ya pili ya
mafunzo kugongana na kalenda ya kuanza mihula ya masomo ya elimu ya
juu", alisema Dk Mwinyi.
Na
kuongeza vijana waliopaswa kujiunga na mafunzo hayo ila hawakujiunga
bila ridhaa ya jeshi, wameingizwa kwenye orodha ya watoro wa jeshi hilo
na kwamba wizara inaangalia uwezekano wa kuiwezesha JKT, kuchukua kundi
hilo wakiwemo watoro, kuanza kwa mkupuo mmoja mafunzo hayo Juni hadi
Agosti mwaka huu.
"Tunatafuta
uwezekano wa kuiwezesha JKT, kuwachukua watoro wa mafunzo hayo na wale
walioshindwa kujiunga kwa kugongana kwa mihula ya masomo, kuingia
mafunzoni kwa mkupuo mmoja kuanzia mwezi Juni hadi Agosti mwaka huu, ili
wawahi muhula wa masomo kwa elimu ya juu", alisema Dk Mwinyi.
Hivyo
aliwataka vijana wote waliohitimu kidato cha sita na kupaswa kujiunga na
JKT, na hawakufanya hivyo bila sababu wala kupata ridhaa ya jeshi hilo
wafahamu wako kwenye orodha ya watoro wa jeshi hilo na kwamba ni lazima
watapaswa kwenda mafunzoni.
Akizungumzia
changamoto zinazokabili utekelezaji wa mafunzo hayo hivi sasa, Dk
Mwinyi alisema ufinyu wa bajeti unasababisha mafunzo hayo kushindwa
kutelekezwa kwa sasa, kwani kuna uhaba wa fedha za kugharamia huduma za
mafunzo pamoja na kushindwa kukarabati majengo ya miundombinu katika
makambi ya jeshi.
Na
kufafanua kuwa fedha zinazotolewa ni kidogo na zinaifanya JKT kuwa
kwenye madeni makubwa na kuishauri serikali itoe fedha za kuwawezesha
kumaliza ukarabati wa kambi zao ili waweze kuwachukua wahitimu wote wa
kidato cha sita kwa mkupuo mmoja, utakaowezesha kumaliza mafunzo mapema
na kujiunga na vyuo vya elimu ya juu kwa wakati.
Alisema
ufinyu huo wa bajeti umefanya pia miradi ya maendeleo kushindwa
kutekelezwa kama bajeti ilivyopitishwa ambapo hadi kufikia robo ya tatu
ya mwaka wa fedha 2014/15 fedha zilizopokewa na wizara hiyo zilikuwa
asilimia 29.5 ya bajeti iliyoidhinishwa.
Na
kufafanua kuwa katika mwaka wa fedha 2014/15 wizara iliomba Sh bilioni
708.7 kwa ajili ya matumizi ya maendeleo lakini hadi kufikia Machi mwaka
huu,fedha zilizoidhinishwa ni Sh bilioni 248.8 ikiwa ni sawa na
asilimia 35.1 ya mahitaji halisi.
Kwa mwaka
wa fedha 2015/16, Wizara hiyo inaomba kuidhinishiwa jumla ya Sh
trilioni 1.7 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na ya maendeleo. (HABARI LEO)
Chapisha Maoni