Musa Mateja
KIBANO! Staa
wa Bongo Fleva mwenye jina kubwa Afrika, Nasibu Abdul ‘Diamond
Platnumz’, juzikati alijikuta kwenye wakati mgumu baada ya ‘kutaitiwa’
kwa saa mbili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere
(JNIA) kisa kikiwa wingi wa mabegi (3) makubwa aliyoshuka nayo akitokea
nchini Afrika Kusini ‘Sauzi’, Ijumaa Wikienda linakupa ‘unyunyuz’ kamili.
Tukio hilo lililoshuhudiwa hatua kwa hatua na gazeti hili, lilijiri Juni
26, mwaka huu kwenye eneo la kukagulia mizigo ya abiria uwanjani hapo
kitendo kilichosababisha Diamond kutokwa na kijasho chembamba.
TAFSIRI YA MABEGI MAKUBWA
Chanzo chetu kilichokuwa ndani ya jengo la kutokea abiria kililiambia Ijumaa Wikienda kuwa,
maafisa ukaguzi wa uwanja huo walimtilia shaka Diamond hivyo
ikawalazimu wayakague mabegi hayo hadi ndani lakini pia walimkuta ana
upungufu wa stakabadhi za mizigo hiyo.
KUHUSU STAKABADHI
Kuhusu stakabadhi zisizokuwepo, ilibidi Diamond ampigie simu ‘mdogo
wake’ (si wa tumbo moja) aliyejulikana kwa jina la Q-Boy ampelekee kwani
alitua nazo Bongo siku moja kabla, yaani Juni 25.
NDANI YA MABEGI
Ndani ya mabegi hayo, kulikutwa kamera, maiki na vifaa vya studio.
IMANI YA WAPEKUAJI
Shuhuda mmoja ambaye Ijumaa Wikienda lilimkuta
nje ya chumba ambacho Diamond alikuwa akipekuliwa, alisema maafisa hao
waliamini msanii huyo alikuwa ameshuka na madawa ya kulevya
‘unga’.“Unajua mastaa siku hizi wanaongoza kwa kubeba unga. Sasa
serikali iko makini nao sana. Ndiyo maana wengi wao wakipita hapa
wanakaguliwa kuliko abiria wengine,” alisema mtu huyo aliyejitambulisha
kuwa ni dereva wa teksi uwanjani hapo.
DIAMOND APIGWA PICHA, AONGEA NA WIKIENDA
Paparazi wetu aliendelea kuganda mlangoni hapo hadi Diamond alipotoka na
kumfotoa picha mbalimbali na baadaye alimfuata hadi kwenye gari aina ya
Toyota Lexus na kumuuliza kama anajua kisa cha kupekuliwa kwa muda
mrefu vile.
“Nilikuwa na mizigo naishughulikia ili itoke hivyo kuna mambo pia
tulikuwa tunapishanapishana pale maana walihitaji nilipie ushuru wakati
vifaa vya studio tulishaambiwa ni ‘free’ (bure). Pia kulikuwa na risiti
za mizigo ambazo zilikuwa hazionekani, kumbe Q-Boy alitangulia nazo jana
mimi nikawa nimesahau.
“Ila wao walikuwa wakijiridhisha kwenye mizigo yangu. Walifikiri nimebeba unga,” alisema Diamond.
HALI YA SASA UWANJANI
Mbali na Diamond kupekuliwa kwa muda mrefu, kwa sasa abiria wanaoingia
na kutoka kwenye uwanja huo wamekuwa wakikaguliwa kwa umakini ili
kubaini uhalali wa mizigo yao lengo kubwa ni kudhibiti uingiaji au
utokaji wa madawa ya kulevya ambapo serikali imeweka umakini katika
kupambana na biashara hiyo haramu.
CHRISTIAN BELLA
Ukiachana na Diamond, mastaa wengine waliowahi kukumbana na pekuapekua
kama hiyo ni Mkurugenzi wa Bendi ya Malaika, Christian Bella na
mtangazaji wa Radio Time FM, Hadija Shaibu ‘Dida’.
Bella yeye alikumbwa na adha hiyo, mwaka juzi, usiku wa saa nane akiwa
anatokea nchini Uturuki na Ndege ya Shirika la Turkish Airways.
Dida naye ilikuwa mwaka 2012 ambapo alikumbwa na pekuapekua hiyo
alipoingia uwanjani hapo kuelekea nchini Thailand kwa shughuli za
kibiashara.
Chapisha Maoni