Historia yake
Dk Willibrod Slaa ni Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema). Slaa alizaliwa Oktoba 29, 1948 kijijini Kwermusi, Wilaya ya
Mbulu (Oktoba atafikisha umri wa miaka 67). Slaa alisoma Shule ya Msingi
Kwermusi iliyoko wilayani Mbulu mwaka 1958-1961 na baadaye Shule ya
Kati (Middle School) ya Karatu kati ya mwaka 1962-1965.
Baada ya darasa la nne, Dk Slaa alijiunga na Seminari ya Dung’unyi
mkoani Singida mwaka 1966-1969 na kusoma sekondari, kisha akaendelea na
masomo ya juu ya sekondari katika Seminari ya Itaga mkoani Tabora mwaka
1970 na 1971, alikohitimu kidato cha sita.
Alipomaliza kidato cha sita katika Seminari ya Itaga alikuwa
amekwishafanya maamuzi ya kufanya utumishi wa kanisa. Alijiunga na
Seminari ya Kibosho mwaka 1972-1973 na kupata stashahada ya Falsafa
iliyompa sifa ya kudahiliwa na Seminari Kuu ya Kipalapala iliyoko Tabora
kati ya mwaka 1974 na 1977 na alipata fursa ya kubobea zaidi katika
masomo ya falsafa na theolojia, huku pia akisoma Stashahada ya Theolojia
katika Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda.
Dk Slaa alianza kuwa kiongozi tangu alipokuwa mwanafunzi pale Kipalapala
ambapo alichaguliwa kuwa Rais wa Wanafunzi, mapadri nilioongea nao
wanasema alikuwa mmoja wa viongozi wazuri sana kupata kuongoza
Kipalapala.
Baada ya safari ndefu ya kuusaka “utumishi wa Mungu” Slaa alipadirishwa
(alipewa upadri rasmi) mwaka 1977 na baada ya utumishi wa miaka michache
alijiunga na Chuo Kikuu cha Pontifical Urbaniana nchini Italia akisomea
udaktari wa Sheria za Kanisa maarufu kama J.C.D. (Juris Canonici Doctor
) au I.C.D. (Iuris Canonici Doctor) kati ya mwaka 1979 na 1981. Katika
mfumo wa Kanisa Katoliki, (J.C.D au I.C.D) ndiyo shahada ya juu kabisa
katika masomo ya sheria ya kanisa.
Dk Slaa amefanya kazi mbalimbali katika taasisi za Kanisa Katoliki
nchini Tanzania. Amewahi kuwa Msaidizi wa Askofu na Mkurugenzi wa
Maendeleo katika Jimbo la Mbulu. Amewahi kuwa Katibu Mkuu wa Baraza la
Maaskofu Tanzania (TEC) kwa muda wa miaka tisa (mihula yote mitatu). TEC
ndiyo chombo cha juu cha usimamizi wa mambo ya Kanisa Katoliki hapa
Tanzania.
Kwa mujibu wa Profesa Kitila Mkumbo, mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam, katika utafiti wake juu ya Dk Slaa, anasema “…Dk.
Slaa anaelezwa kama Katibu Mkuu mwenye ufanisi mkubwa zaidi tangu TEC
ianzishwe. Miundombinu mingi ya Kanisa Katoliki nchini ilianzishwa na
kukamilishwa katika kipindi ambacho Dk Slaa alikuwa Katibu Mkuu wa TEC.”
Dk Slaa alijitoa kwenye upadri mwaka 1991. Kwa mujibu wa taarifa za
maaskofu kadhaa nilioongea nao, wanasema “Dk Slaa lifanya hivyo kwa
kufuata taratibu kamili ndani ya Kanisa Katoliki na aliacha yeye
mwenyewe bila kushinikizwa, kufukuzwa au kupewa onyo”.Mara kadhaa Dk
Slaa alipoulizwa kwa nini aliamua kuachana na upadri, amekuwa
akikaririwa akisema kwamba “kuna mambo ambayo alidhani dhamira yake
ilipingana nayo na akaona asingeliweza kuendelea, japokuwa anasisitiza
kuwa masuala hayo ni binafsi zaidi.”
Ndani ya Chadema amewahi kushikilia wadhifa wa Makamu Mwenyekiti, kabla
hajachaguliwa kuwa Katibu Mkuu katika mwaka ambao Freeman Mbowe
alichaguliwa kuwa mwenyekiti na wameendelea kuongoza kwa pamoja hadi
hivi sasa.
Dk Slaa ni mwandishi mzuri wa vitabu, ameandika vitabu vitatu ambavyo ni
Utimilifu wa Msichana (1977), Utimilifu wa Mvulana (1977) na Expediency
and Exigency Liturgical Legislation (1981). Pia, kiongozi huyu
anazungumza lugha nane kwa ufasaha; Kiswahili, Kiingereza, Kilatini,
Kiitaliano, Kijerumani, Kihispania, Kireno na Kifaransa.
Dk Slaa aliwahi kumuoa Rose Kamili na kuzaa naye watoto wawili, Emiliana
Slaa na Linus Slaa lakini waliachana muda mfupi kabla ya Uchaguzi Mkuu
wa mwaka 2010. Hivi sasa anaishi na “mchumba wake” Josephine Mushumbushi
na wamepata mtoto mmoja.
Mbio za ubunge
Dk Slaa aliingia kwenye kinyang’anyiro cha ubunge kwa mara ya kwanza
mwaka 1995, akiomba ridhaa ya kuwatumikia wananchi wa jimbo la Karatu
mkoani Arusha kwa tiketi ya CCM na alishinda kwenye kura za maoni za
chama hicho. Vikao vya CCM vilipokutana Dodoma vikamuengua na kumuweka
mbunge aliyekuwa anamaliza muda wake, Patrick Qorro. Wananchi wa Karatu
wameniambia kuwa iliwapasa wamshinikize Dk Slaa kuchukua fomu na
kugombea ubunge kupitia chama kingine. Bahati ikakidondokea Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Dk Slaa alipambana na wagombea kutoka vyama vinne; CCM, UDP, CUF na NCCR
na aliwashinda wote kwa kupata asilimia 52.6, akifuatiwa na Patrick
Qorro wa CCM aliyepata asilimia 44.1. Kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka
2000, Dk Wilibrod Slaa alishiriki kwenye uchaguzi akigombea kutokea
Chadema kwa mara pili na kupata ushindi mkubwa zaidi kuliko mwaka 1995
na aliongoza hadi mwaka 2000. Na kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 pia
aligombea ubunge kwa mara ya tatu jimboni Karatu na kushinda kwa
asilimia 50.65 dhidi ya asilimia 49.0 za Patrick Tsere wa CCM.
Kati ya mwaka 2005– 2010 naweza kusema kuwa Dk Slaa ndiye alikuwa shujaa
wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na namuona kama mbunge
aliyefanya kazi kubwa kitaifa na kimataifa kushinda mbunge mwingine
yeyote. Huu ndiyo wakati ambapo yeye na Zitto Kabwe na wabunge wengine
wachache walikuwa mwiba usioshikika bungeni. Hoja zao nzito kuhusu
ufisadi, rushwa, uwajibikaji duni wa serikali vilimfanya kila Mtanzania
aone nini maana na umuhimu wa Bunge la Wananchi.
Mbio za urais
Dk Slaa aliteuliwa na Chadema kugombea urais wa Tanzania katika Uchaguzi
Mkuu wa Mwaka 2010. Kwa sababu ya umahiri wake wa kujenga hoja na
kuonyesha kuwa ana uwezo wa kipekee, aliibuka katika nafasi ya pili,
akipata asilimia 27.05 za kura zote, kwa kuachwa na Jakaya Kikwete wa
CCM aliyeongoza kwa kupata asilimia 62.83.
Kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu 2015, Dk Slaa ni mmoja wa wanasiasa
mahiri kutoka ndani ya vyama vya upinzani ambao wanatajwa kuwa na sifa,
uwezo na vigezo vya kuongoza nchi.
Nguvu yake
Jambo la kwanza ambalo linampa nguvu Dk Slaa ni elimu yake. Huyu ni
kiongozi mwenye stashahada tatu pamoja na shahada ya Uzamivu (PhD).
Anayo Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Sheria ya Kanisa kutoka Chuo Kikuu
cha St. Urban, Rome. Pia ana stashahada ya Theolojia kutoka Kipalapala
Seminari, Stashahada ya falsafa kutoka Kibosho Seminari, Stashahada ya
Afya ya Macho kutoka Kituo cha Kimataifa cha Macho.
Pamoja na kwamba hakusoma katika mfumo wa kiserikali zaidi hapa Tanzania
na amekuwa “Padri” katika kanisa, kwa kiasi kikubwa masuala ambayo
ameyasimamia kutokana na elimu yake yamekuwa ya kijamii, kisiasa,
kiuchumi na kimataifa zaidi. Mapadri wengi husoma falsafa na hawana
tofauti yoyote na wasomi wa kawaida wanaosoma falsafa vyuoni na baadaye
kuajiriwa katika kazi za kawaida.
Pili, Dk Slaa ana sifa kubwa sana katika kufanya kazi kwa juhudi
“kuchapa kazi”. Mimi nimefanya naye kazi kwa miaka kama miwili hivi
katika mazingira tofauti. Nimeshuhudia namna ambavyo hawezi hata kutoka
nje kunyoosha mgongo kama mko vikaoni, mnaweza kujadiliana kutwa nzima
na mkatoka hapo kukimbizana mahali kuhutubia wananchi asinywe hata maji.
Slaa ana uwezo mkubwa sana kwenye eneo hili na kwa hakika nadhani nchi
inahitaji Rais anayechapa kazi kufa au kupona.
Nguvu ya tatu ya kiongozi huyu ni uadilifu. Dk Slaa amewahi kufanya kazi
katika maeneo mengi tu tangu akiwa Padri wa Kanisa Katoliki, hadi
amekuwa mbunge kwa miaka 15 huku akiongoza Kamati ya Bunge ya Serikali
za Mitaa. Hata mara moja hatukuwahi kusikia harufu, tuhuma au maneno
kuwa amekwapua “senti” za umma au amechukua fedha za rushwa mahali. Kazi
alizofanya ni safi na salama na zinampa “mamlaka ya kimaadili” (moral
authority) kusimama hadharani na kusema kuwa atapambana na rushwa na
ufisadi. Naamini, watu wa aina yake, kwa sasa ni muhimu sana katika nchi
na uongozi wa nchi.
Nne ni kuheshimika na umaarufu. Dk Slaa ni mmoja wa viongozi wa upinzani
wanaoheshimika na kufahamika sana hapa nchini Tanzania. Lakini pia sifa
hizo zinavuka mipaka ya Tanzania ambako nako amefanya kazi za utumishi
muda mrefu huku akiendelea kupata mialiko mikubwa ya nchi kama Marekani,
nchi za Ulaya, ambako amekaribishwa katika vyuo vikuu bora kabisa
duniani na kutoa mihadhara. Kwa hiyo anatambulika na kuheshimika kama
mmoja wa Waafrika wanaotoa mchango mkubwa katika kuleta mabadiliko na
maendeleo ya jamii zao. Sifa za namna hii ni nguzo muhimu kwa mtu
anayetajwa kuwa na vigezo vya urais.
Udhaifu wake
Udhaifu wa Dk Slaa uko kwenye eneo la uchujaji wa taarifa anazopewa juu
ya masuala mbalimbali na hata kuzifanyia maamuzi sahihi. Kwa kipindi
kirefu nimekuwa nikimfuatilia kiongozi huyu na kugundua kuwa hapendi
kutumia muda mrefu kuchuja taarifa anazoletewa kabla ya kuzitolea
matamko au kuzichukulia msimamo. Hali hii imesababisha mara kadhaa (si
nyingi) asikike akitoa taarifa za masuala ambayo yalikuja kuonekana
kinyume au hayakuwa sahihi. Kwa mfano, katika kampeni za mwaka 2010
aliwahi kushutumu kuwa “…lori moja katika Wilaya ya Tunduma limekamatwa
na masanduku ya kupiga kura”. Alipewa taarifa hizi na wasaidizi wake na
kuzitangaza. Kwa bahati mbaya hazikuwa taarifa sahihi.
Pili, kuna wakati aliwahi kutangaza kwamba mgombea wa CCM, Rais Jakaya
Kikwete alikuwa ameonekana katika Hoteli ya Lakairo Jijini Mwanza akiwa
anapanga mikakati ya kuiba kura na wana CCM wenzake. Ilikuja kuthibitika
kuwa wakati, tarehe na muda alioungea, Kikwete hakuwa mkoani Mwanza
Na tatu, akiwa katika mkutano wa hadhara mjini Shinyanga, Dk Slaa
aliwahi kutangaza kuwa aliyekuwa mkuu wa mkoa huo alikuwa amefariki
dunia. Hali hiyo ilileta mshtuko kwa wananchi na wanafamilia, lakini
baadaye ilithibitika kuwa mkuu huyo wa mkoa alikuwa hai. Taarifa hii Dk
Slaa aliitangaza baada ya kuambiwa na msaidizi wake alipokuwa jukwaani.
Tabia ya Dk Slaa ya kuwaamini sana wasaidizi wake si jambo zuri na
linaweza kuwa na madhara makubwa, ikiwa hataanza kujipa muda na kuchuja
taarifa kabla ya kuzitoa ili kumuondoa kwenye dhana ya kujenga “masuala
tata” au kutuhumiwa na wapinzani wake kisiasa, kwamba hasemi ukweli.
Lakini pia, tabia ya namna hii inaweza kumsababishia mara kadhaa afanye
maamuzi yasiyo sahihi kwa sababu tu ya kuambiwa mambo yasiyo kweli na
akaweka imani mbele kuliko utafiti na kujiridhisha kwanza. Sehemu ya
udhaifu niliyoitaja hapa, imewahi pia kutajwa na Mhadhiri Maarufu wa
Chuo Kikuu na kwa bahati mbaya yakawa yamegongana na mawazo yangu juu ya
Dk Slaa.
Nini kinaweza kumfanya apitishwe?
Kisiasa na kwa wananchi, Dk Slaa ndiye mwana Chadema anayekubalika
kuliko viongozi wote wa chama hicho. Naamini kuwa vikao vya kitaifa vya
chama chake vitaitumia hii kama sababu muhimu ya kumpa fursa ya kugombea
urais ili kuwasogezea wananchi chaguo muhimu.
Pili, Dk Slaa amegombea urais mwaka 2010 na kuibuka nafasi ya pili
akipitwa na mgombea wa CCM tu. Kumpeleka kuchuana na wenzake ndani ya
Ukawa huenda kukaifanya pia Ukawa izingatie suala hilo na kumuona kama
mgombea muhimu kwa wakati wa sasa.
Nini kinaweza kumwangusha?
Kwa mtizamo wangu, ni jambo moja tu ndilo huenda linaweza kumfanya Dk
Slaa asivuke vizingiti ndani ya Chadema, jambo hili ni ikiwa Chadema
haitapewa fursa ya kuweka mgombea urais ndani ya Ukawa.
Tukumbuke kuwa ndani ya Ukawa kuna vyama vingine kama CUF, NCCR na NLD
ambamo pia katika baadhi ya vyama hivyo kuna wagombea wenye sifa nzito
na za kupigia mfano na huenda kushinda za Dk Slaa. Ikiwa Chadema
haitapewa fursa ya kuweka mgombea urais kwa sababu ya kutoa nafasi hiyo
kwa vyama vingine, ni dhahiri kuwa nafasi ya Dk Slaa kugombea urais
mwaka huu itakuwa imefikia mwisho.
Asipochaguliwa (Mpango B)
Mambo matatu yanaweza kuwa mezani kwa Dk Slaa ikiwa hatagombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama chake:
Jambo la kwanza ni kuendelea kusimamia ukuaji wa Chadema. Dk Slaa
amekuwa ndiye Katibu Mkuu wa chama hicho aliyepata mafanikio kuliko
makatibu wakuu wengine waliowahi kusimamia chama. Ikiwa hagombei urais
nadhani ataendelea na jukumu kubwa la kukijenga chama chake kwa ufanisi
mkubwa zaidi.
Jambo la pili linaloweza kuwa mezani ni kugombea ubunge. Dk Slaa
alifanya kazi kubwa sana katika mabunge yaliyopita, hususani Bunge la
2005 – 2010. Itakuwa jambo la kusikitisha sana kama hagombei urais
halafu hagombei pia ubunge. Haya yatakuwa matumizi mabaya ya rasilimali
watu zilizoko kwenye vyama vya upinzani “misuse of human resources in
opposition political parties”. Vyama vya upinzani vinapaswa kuachana na
kasumba za zamani za kujijengea watu fulani kama “presidential
materials” tu na kusahau kuwa watu hao wana jukumu kubwa la kusimamia
serikali moja kwa moja kama hawagombei urais.
Na mwisho, namuona Dk Slaa kama Waziri Mkuu mahiri na thabiti kabisa
kwenye serikali ya Ukawa, ikiwa vyama hivyo vitashinda uchaguzi wa mwaka
huu na kuongoza serikali na ikiwa hatokuwa mgombea urais na au Rais
Mteule, atakuwa na sifa za kipekee, uzoefu wa kutosha wa kibunge,
masuala ya kitaifa na kimataifa na bila shaka anaweza kabisa kuongoza
serikali imara kama Waziri Mkuu.
Hitimisho
Nilipokuwa nafanya utafiti juu ya Dk Slaa pia sikupata matatizo yoyote,
ilikuwa ni kazi nyepesi sana kwa sababu nimemfahamu na kumfuatilia kwa
kipindi kirefu kilichopita. Kiongozi huyu ana mambo mengi sana ya kuiga
kutoka kwake, misimamo yake, utendaji kazi wake, uadilifu, weledi wa
masuala ya kijamii na usimamizi.
Haya yote yanamvusha katika wasiwasi wa Watanzania kuwa huenda vyama vya
upinzani havina viongozi thabiti wa kuongoza dola. Mimi nasema viongozi
hao wapo na Dk Slaa ni mfano mojawapo. Kwa yote haya, namtakia kila la
heri kiongozi huyu, kwamba safari yake kisiasa iwe na mafanikio mema kwa
jamii na taifa letu.
Mwananchi
Chapisha Maoni
Click to see the code!
To insert emoticon you must added at least one space before the code.