WAZIRI wa
Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, ambaye pia anaomba
CCM impitishe kuwa mgombea urais katika Uchaguzi Mkuu baadaye mwaka huu,
Bernard Membe amekiri kwamba katika kinyang’anyiro cha urais ndani CCM,
mtu anayemnyima usingizi ni Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
Akizungumza
na wanachama waliojitokeza kumdhamini jana, Membe alisema Pinda
asingechukua fomu ya urais ndani ya CCM, angefurahia ushindi tu na
tayari angekuwa ameshona suti na kushangilia ushindi.
Alisema
kuwa Waziri Mkuu Pinda ni mchapakazi, asiye mbinafsi, mwadilifu,
mvumilivu sana mwenye hekima na busara ya hali juu, mwanasheria
aliyebobea na ndiye mwalimu aliyemfundisha kazi.
“Wengine
wote hawanitishi nitawagonga lakini nikifika kwa Pinda itabidi nipumue
kwanza...kwa hiyo mimi na Pinda ni pacha nikishindwa mimi nitamuunga
mkono lakini akishindwa naamini ataniunga mkono, ndio maana hata wakati
nakuja huku nimewasiliana naye akanieleza nenda na amenisaidia nimepata
wadhamini wa kutosha,” alisema.
Membe
amesema kuwa Mungu akimjaalia kuteuliwa na CCM kushinda urais
atahakikisha baadhi ya miradi inayotumia fedha za ndani ambayo inasuasua
ikiwemo ujenzi wa barabara ya Sumbawanga hadi Mpanda unakamilika,
lakini pia bonde la Ziwa Rukwa linatumika kuzalisha chakula ambacho
kitalisha nchi nzima kwa kuwa ardhi yake ina rutuba na inafaa kwa
kilimo.
Pia,
Membe aliwaasa baadhi ya wanaCCM kuacha kuwashangilia kila mgombea
anayepita kuomba udhamini kwa kuwa si wote wana sifa kwani wenye sifa
stahiki ni yeye na Waziri Mkuu Pinda.
Awali,
Katibu Mwenezi wa Mkoa huo, Clement Bakali alisema kuwa mgombea huyo
amepata wadhamini 855 kutoka wilaya zote za mkoa wa Rukwa.
Chapisha Maoni