0
Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Taaluma, Profesa George Shumbusho (kulia) akiwasilisha mada wakati wa kongamano la majadiliano ya rasimu ya mtaala wa Chuo Kikuu Mzumbe, Skuli ya Biashara, hivi mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam. Kongamano hilo lilihusisha wadau mbalimbali kutoka sekta ya umma na binafsi.
Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Taaluma, Profesa George Shumbusho (kulia) akijadiliana jambo na Mkuu wa Skuli ya Biashara ya chuo hicho, Dr. Hawa Tundui (kushoto) wakati wa kongamano la majadiliano ya rasimu ya mtaala wa Skuli hiyo ya Biashara mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam. Kongamano hilo lilihusisha wadau mbalimbali kutoka sekta ya umma na binafsi.
Chuo Kikuu Mzumbe kimeanza rasmi awamu ya pili ya mchakato wa kuhuisha mtaala unaotumika katika Skuli yake ya Biashara ili kuendana na hali hasi ya mabadiliko yanayotokea haraka nchini na duniani katika nyanja za siasa, uchumi, jamii na teknolojia.
Inatarajiwa kuwa mabadiliko hayo yatasaidia pia kuwajengea zaidi uwezo wahitimu wa chuo hicho kujiajiri na kuajiriwa kwa urahisi zaidi.
Kaimu Naibu Makamu mkuu wa Chuo hicho, Taaluma, Profesa George Shumbusho aliwaambia waandishi wa habari mwishoni mwa wiki mjini hapa kuwa mabadiliko hayo yanalenga kutoa wahitimu watakaokuwa na uwezo wa kushindana kitaifa na kimataifa katika nyanja za biashara, manunuzi, na ujasiriamali.
Uongozi na wataalamu wa chuo hicho ulikutana na wadau mbalimbali kutoka sekta ya umma na binafsi kupitia rasimu ya mapendekezo ya mabadiliko ya mtaala wa skuli ya chuo hicho.
“Ni utaratibu wa chuo chetu kuhakikisha kuwa tunapitia mitaala kila baada ya miaka mitatu ili kuihuisha,”alisema Prof. Shumbusho.
Alisema mwanzo skuli hiyo iliwaomba wadau wa chuo wakiwemo waajiri, wazazi na taasisi mbalimbali kutoa mawazo yao kuhusu hitaji la kuwa na mtaala mpya unaoendana na mabadiliko yanayojitokeza hapa nchini na ulimwengu kwa ujumla.
Maoni hayo yalichukuliwa na kuingizwa katika rasimu ya mtaala iliyopendekezwa na kupitiwa na walimu na wanafunzi ambao waliandaa rasimu ya pili ambayo ndio ilikuwa inajadiliwa tena na wadau hao.
Profesa Shumbusho alisema baada ya kupata maoni ya wadau hao tena, watatoa rasimu ya mwisho ambayo itajadiliwa na seneti ya chuo hicho na kupelekwa Tume ya Vyuo vikuu (TCU).
Inatarajiwa kuwa mtaala huo utaanza kutumika mwezi Octoba 2015.
Mkuu wa Skuli ya Biashara, Dkt. Hawa Tundui alisema skuli hiyo imedhamiria kutoa elimu iliyo bora na kuwa shindani hapa nchini na katika eneo hili la Afrika.
“Tunataka kuleta manufaa zaidi kwa wahitimu, jamii, na nchi kwa ujumla,” alisema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB), Dkt. Clemence Tesha alisema mitaala ni lazima iendane na mageuzi yanayojitokeza la sivyo vyuo vitakuwa vinafundisha vitu vilivyopitwa na wakati.
“Katika vyuo hili ni jambo la lazima ili kuiwezesha nchi kuwa na wasomi wanaoendana na wakati,”alisema.
Alisema wao kama wadau wametoa maoni yao kwa mambo ya msingi yanayohitajika kufanyika ili taifa liweze kuwenda sambambana na mahitaji ya soko na nchi.
Baadhi ya wadau walioshiriki katika kujadili rasimu hiyo ni pamoja na Wizara ya Maji, Ofisi ya Waziri Mkuu, Bodi ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), PSPTB, Mamlaka ya Manunuzi nchini (PPRA), Mamlaka ya Usimamzi na Udhibiti wa Huduma za Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA), benki ya CRDB, Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu, Kampuni za Ukaguzi, na wajasilimali mbalimbali.(Muro)

Chapisha Maoni

 
Top