Viongozi wa CUF
Kwa ufupi
Vyama vinavyounda Ukawa ambavyo ni Chadema, CUF, NLD na NCCR-Mageuzi
vilisaini makubaliano ya kushirikiana katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika
Oktoba 25By Raymond Kaminyoge, Mwananchi
Dar es Salaam. Chama cha Wananchi (CUF) kinafanya kikao chake cha Baraza
Kuu la Uongozi leo mjini Zanzibar huku wafuasi wa vyama vinavyounda
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wakisubiri kwa hamu kitakachoamuliwa
kuhusu mgombea urais wa umoja huo.
Vyama vinavyounda Ukawa ambavyo ni Chadema, CUF, NLD na NCCR-Mageuzi
vilisaini makubaliano ya kushirikiana katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika
Oktoba 25, mwaka huu kwamba vitamsimamisha mgombea mmoja katika nafasi
ya rais, ubunge na udiwani.
Hata hivyo, wakati viongozi wa vyama hivyo wakiwa katika vikao vya
uteuzi wa nafasi ya rais atayepeperusha bendera ya Ukawa, CUF walikaa
kando wakisema wanasubiri uamuzi wa kikao cha Baraza Kuu la uongozi
linaloketi leo ili kuendelea na mchakato huo.
Hatua hiyo ilisababisha sintofahamu na zilienea habari kwamba CUF
wamejitoa. Lakini Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara), Magdalena Sakaya
aliwaambia waandishi wa habari kwamba wao bado wamo ndani ya Ukawa
isipokuwa wanasubiri kupewa Baraka na Baraza Kuu la Uongozi.
Sakaya alifafanua kwamba Baraza hilo litajadili na kutoa uamuzi ili wanaposhiriki vikao vya Ukawa wawe kitu kimoja.
Juzi, katika mkutano wa Chadema uliofanyika jijini Mwanza, Naibu Katibu
Mkuu wa Chadema (Bara), John Mnyika na yule wa Zanzibar, Salim Mwalimu
walisema chama hicho kinasubiri hatima ya kikao cha wenzao wa CUF
kinachofanyika ili waweze kumtangaza mgombea urais wa Ukawa.
Akizungumza na gazeti hili jana, Sakaya alisema kikao hicho cha siku
moja kitafanyika leo kama kilivyopangwa mjini Zanzibar na ajenda
zitakuwa masuala ya Ukawa na hasa nafasi ya mgombea wa nafasi ya urais.
Alisema ajenda nyingine ni kujadili na kuwapitisha wagombea wa nafasi za ubunge na udiwani.
“Kikao kitajadili masuala ya ndani ya chama na tutawapa taarifa kuhusu yatakayoamuliwa baada ya kikao,” alisema.
Aidha, habari za ndani zinasema kikao hicho kitajadili shughuli
inayoendelea ya uandikishaji wapigakura kupitia mfumo wa Biometric
Voters Registration (BVR). Hatua hiyo inatokana na matatizo mbalimbali
yaliyojitokeza wakati uandikishaji hali iliyosababisha baadhi ya watu
kushindwa kujiandikisha na hivyo kukosa haki yao ya kupiga kura.
Wafuasi wa vyama hivyo na Watanzania kwa ujumla wanasubiri kusikia jina
la mgombea wa Ukawa hasa baada ya CCM kumtangaza Waziri wa Ujenzi, Dk
John Magufuli kuwa mgombea wake wa urais.
Chapisha Maoni