WATIA nia
wanne waliochukua fomu za kuwania kuteuliwa na Chama Cha Mapinduzi
(CCM) kuwa wagombea wa kiti cha urais wametupwa nje ya mchakato huo,
baada ya kushindwa kurudisha fomu.
Walioshindwa
kurudisha fomu hizo mpaka muda wa mwisho ulipofika saa 10.00 jioni jana
ni Peter Nyalali, Helena Elinewinga, Anthony Chalamila na Dk Muzamil
Kalokola.
Mmoja wa
watia nia hao, Helena mara baada ya kuchukua fomu Juni 25, mwaka huu,
alikwenda kumtembelea mmoja wa maofisa wa chama hicho akitafuta ushauri
wa namna ya kufanya ili kupata udhamini, lakini baadaye aliamua
kutelekeza fomu hizo bila kuondoka nazo.
Jumla ya
wanachama 42 walijitokeza kuchukua fomu kwa ajili ya kuomba uteuzi huo
ambapo walitakiwa kuwa na wadhamini 450 kutoka mikoa 15, ikiwemo mitatu
ya Zanzibar.
Katika
mkutano wake na waandishi wa habari jana, Naibu Katibu Mkuu wa CCM
Tanzania Bara, Rajab Luhwavi alisema zoezi la kuchukua fomu lilianza
Juni 3, mwaka huu na lilitarajia kumalizika Julai 2 saa 10.00 jioni.
Alisema
zoezi hilo limefanyika kwa utulivu ambapo kati ya wanachama 42
waliochukua fomu na kutakiwa kuwa na wadhamini kutoka mikoa 15 ikiwemo
mitatu ya Zanzibar ambapo kati ya hao ni 38 ndio waliofanikiwa kurejesha
fomu.
Alisema hatua itakayofuata ni mchakato wa vikao vya chama kuanzia Jumanne wiki ijayo.
“Mmoja wa
wachukua fomu, Helena Elinawinga alitelekeza fomu hizo kwa mmoja wa
maofisa wa CCM baada ya kufika kuomba ushauri huku akitaka kupewa kwanza
elimu ya siasa kabla ya kuanza kutafuta wadhamini,” alisema Luhwavi.
Sita warejesha fomu
Wakati
makada wanne washindwa kurejesha fomu hizo, wenzao sita waliwahi muda
uliowekwa wa kurejesha fomu na wakawa na sifa za kujadiliwa na vikao vya
maamuzi.
Ngeleja na mambo 15
Wa kwanza
kurudisha fomu hizo alikuwa ni Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja
ambaye aliendelea kusisitiza kuwa CCM wamtafakari kwa mambo 15
aliyoyafanya wakati akiwa waziri wa nishati na madini.
Ngeleja,
ambaye alirudisha fomu saa 4.45 asubuhi ambaye hata hivyo hakutaja mambo
hayo 15, alisema yeye ni kiongozi makini na Watanzania hawatajuta ikiwa
atachaguliwa kuongoza nchi.
“Nina
maono ya ndoto, CCM ni chama kikongwe ndoto zangu si za mchana
ninayoyatafakari tayari yamefanyika nchi nyingi duniani,” alisema.
Alisema
taifa limekuwa likijengwa na makundi ya wafanyakazi, wakulima na
wafugaji ambapo makundi hayo uanabena taswira nzima na kama taifa
linatakiwa kupiga vita umaskini, maradhi na ujinga.
Alisema
ni lazima kuendeleza juhudi zinazofanywa na wajasiriamali na wanamichezo
pamoja na wasanii kwani ni kundi kubwa na limekuwa likiingiza kipato
kutokana na shughuli wanazofanya.
“Iwapo
nitachaguliwa nitaendeleza sekta za kilimo, ufugaji na uvuvi,” alisema.
Alisema kilimo kimebeba Watanzania asilimia 75 na kama taifa ni muhimu
kuwekeza kwenye kilimo na kuondokana na kilimo cha kutegemea mvua na
badala yake kujikita kwenye kilimo cha umwagiliaji.
Balozi Patrick Chokala
Patrick
Chokala alirudisha fomu saa 11.29 jioni na kusema kitendo chake cha
kuchukua fomu na kukamilisha kutafuta wadhamini ni kuwa amedhamiria na
ana uwezo wa kuongoza serikali ana uzoefu na hakuna geni kwake.
Pia ana
uwezo wa kuendeleza uhusiano wake wa kimataifa kwani elimu yake ni ya
chuo kikuu na kama rais wa Tanzania atadumisha umoja na ushirikiano
hatayumbishwa na mtu yeyote yule na kuondoka katika misingi ya
Watanzania.
“Sina
hulka ya udikteta na ufashisti na wananchi wasiwe na wasiwasi
wataendelea kwa umoja,” alisema. Pia atakuwa mtetezi wa wanyonge kwani
chama hicho ni cha wakulima na wafanyakazi na ataangalia watu wa chini.
Alisema
ni viongozi wajinga wanasisitizia mambo yasiyo ya lazima na kusahau kule
chini kwenye kiatu. Alisema ana ujasiri mkubwa wa kupambana na udhalimu
kwa wananchi.
“Mimi
ninastahili kuwa Rais wa nchi kwani nina uwezo na uzoefu wa kuongoza
serikali, pia kuendeleza ushirikiano wa kimataifa,” alisema. Alisema
atadumisha umoja na kwamba hatayumbishwa na yoyote katika masuala ya
msingi.
Banda Sonoko
Sonoko yeye alirejesha fomu na kusema kuwa fomu moja ya mkoa wa Iringa haijafika na kama itafika kabla ya saa 10 atairejesha.
Alisema
kutafuta wadhamini kulimpa wakati mgumu juu ya namna ya mawasiliano na
kukusanya wanachama kwa ajili ya kuwatoa na kuwapeleka kwenye ofisi za
chama.
Alisema
akipata nafasi ya kuwa rais wa nchi hatotoa kipaumbele kwa nchi
kuendeshwa kwa fedha za wahisani na pia atatoa uhuru wa habari ili jamii
ijengeke kiuelewa. Pia alisema ataendeleza mazuri ya Jeshi la Magereza
kwa kupunguza idadi kubwa ya wafungwa.
“Nitaanzisha
magereza mbadala ya wafungwa nyumbani ambapo watakuea wakiripoti
serikali za mitaa kila siku na kufanya shughuli za kijamii katika maeneo
ya jirani, wateja wa magereza watakuwa watu wenye mashauri ya jinai,”
alisema.
Kwa
upande wa elimu alisema ataanzisha shule ya mfano itakayoanzia chekechea
hadi chuo kikuu na kwamba itakuwa na masomo matatu ya kiswahili, uraia
na utaalamu wa hesabu ili nchi ipate wataalamu waliobobea.
Godwin Mwapongo
Kwa upande wake, Mwapongo alisema amekamilisha mikoa yote 15 na hakuombwa chochote wakati wa kutafuta wadhamini mikoani.
Alisema
atapambana na rushwa kwa kuwarudishia wananchi madaraka na hivyo
wataweza kupambana na rushwa uso kwa uso. Alisema lazima mamlaka
yarudishwe kwa wananchi ili wawe na uwezo wa kudhibiti rushwa.
Alisema
iwapo atachaguliwa atarudisha Azimio la Arusha, lakini si kwa ajili ya
kunyang’anya mali za watu, lakini mali ambayo haikupatikana kwa njia
zisizo sahihi si baraka.
Alisema
wale ambao walinyang’anywa wakati huo ambao bado wako watarudishiwa mali
zao. Alisema akiwa Rais hatakubali kuwa Mwenyekiti wa CCM kwani kuwa na
kofia mbili hakuna nafasi za kuhoji.
Ritha Ngowi
Ngowi kwa
upande wake CCM ilimpa ushirikiano na hivyo kumwezesha kupata wadhamini
bila tatizo lolote. Alisema maeneo mengine walijitokeza kwa wingi,
jambo ambalo lilimpa moyo sana.
Ngowi alisema alizunguka mikoa 15 na ametimiza yote aliyotakiwa kutimiza.
January Makamba
Makamba
yeye amekitaka chama chake, kuteua mgombea atakayewakilisha chama hicho
kwa nafasi ya urais kwa kuzingatia busara za waasisi wa chama hicho,
akiwemo Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Amesisitiza
kuwa Watanzania na wanachama wa chama hicho wanataka wagombea wa CCM
kwa nafasi za ngazi zote ambao wana mvuto kwa watu na ambao itakuwa
rahisi kuwanadi bila kuwatolea maelezo au utetezi kwanza.
January
aliyasema hayo, mjini Dodoma, mara baada ya kuhitimisha ziara yake ya
kutafuta wadhamini katika baadhi ya mikoa nchini pamoja na kurejesha
fomu ya kuomba kugombea Urais kupitia chama hicho tawala.
Alisema
mwaka 1995, Mwalimu Nyerere wakati akihutubia mkutano mkuu wa chama
hicho wa kumteua mgombea Urais wa CCM, alisema kwamba, “Watanzania
wanataka mabadiliko. Wasipoyapata ndani ya CCM, watayatafuta nje ya
CCM”.
Aidha
alisema naye Mwenyekiti na Rais mstaafu wa chama hicho, Benjamin Mkapa,
wakati akihutubia mkutano mkuu wa CCM wa kumteua mgombea Urais wa CCM
mwaka 2005, alisema ni muhimu CCM ikatazama aina ya wapiga kura waliopo,
ambao wengi ni vijana, na kuwapatia mgombea anayeendana nao.
“Miaka 20
baadaye, kauli ile ya Mwalimu na miaka 10 baadaye kauli ya Mkapa bado
ziko sahihi. Katika uchaguzi wa mwaka huu, CCM inayo nafasi ya kuwapa
Watanzania aina ya mgombea anayeashiria na kuakisi mabadiliko
wanayoyataka watanzania,” alisisitiza.
Alisema
ana imani kuwa mchakato wa kumpata mgombea urais kupitia chama hicho,
utazingatia busara hizo za zilizofanya chama hicho, kupata wagombea
sahihi mwaka 1995 na 2005.
“Nina
imani kubwa na viongozi wakuu wa chama chetu katika kutuongoza kupata
mgombea anayeakisi hadhi, heshima na dhamana ya chama chetu,” alisema.
Alisema
pia Rais na Mwenyekiti mstaafu, Mzee Ali Hassan Mwinyi, alipata kusema,
“kila zama na kitabu chake”. Na kusisitiza kuwa umri sio sifa ya uongozi
lakini uongozi unaenda kwa rika au kizazi.
Alisema
kila kizazi kina wakati wake, kila zama zina changamoto na mahitaji yake
na kila kizazi kina wajibu mahsusi wa kukabiliana na changamoto za
wakati wake.
“Vizazi
vilivyopita vya viongozi wetu vimeiongoza nchi yetu vizuri na mafanikio
yako dhahiri. Baada ya miaka zaidi ya 50 ya uhuru, sasa ni wakati wa
kizazi kingine kitakachokuja na fikra mpya, mtazamo mpya na majawabu
mapya kwa changamoto za sasa,” alisisitiza.
Kwa
upande wake, alisema ameshapima na kujitafakari na anaamini ameandaliwa
vizuri kiuongozi na kimaadili kwenye chama, Serikali, bungeni katika
utumishi wake Ikulu.
Chapisha Maoni