Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda, amekataa ombi la wakazi wa jimbo lake la uchaguzi
la Katavi la kumtaka agombee tena ubunge katika jimbo hilo ili
kuendeleza mipango ya maendeleo aliyoianzisha.
Taarifa
iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari ilimnukuu Pinda akijibu maombi ya
wakazi hao baada ya Ibada ya Jumapili iliyofanyika katika Kigango cha
Kanisa Katoliki cha Kibaoni Wilaya ya Mlele mkoani Katavi.
Pinda
alisema anamshukuru Mungu kwa nafasi aliyopewa ya kulitumikia Taifa
akiwa Waziri Mkuu kwa miaka minane na anaamini wakati umefika wa yeye
kuwaachia wengine nafasi ya ubunge wa Jimbo la Katavi.(P.T)
Alisema
ataendelea kuwa karibu na wakazi wa jimbo hilo wakati wote na kwa vile
atakuwa na muda wa kutosha kushiriki kikamilifu katika mikakati ya
kuwaletea maendeleo ili wajikwamue kutoka kwenye umaskini.
Kwa
upande mwingine, Pinda aliwaasa wakazi wa jimbo hilo wawe makini
kuchagua mbunge na madiwani na kamwe watoa rushwa na wabadhirifu
wasipewe nafasi katika uchaguzi ujao utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Akimshukuru
Waziri Mkuu, Paroko wa Parokia ya Usevya wilayani humo, Padri Aloyce
Nchimbi, aliwaasa wakazi wa Mlele kumuenzi Pinda hata atakapokuwa
amestaafu kwani bado watahitaji busara na uzoefu wake katika kujiletea
maendeleo.
Pinda
yuko kijijini kwake Kibaoni ajili ya mapumziko mafupi na alitoa msimamo
wake huo jana ikiwa ni siku ya mwisho kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
kutoa na kupokea fomu kwa makada wake wanaoomba wateuliwe kugombea
ubunge na udiwani katika uchaguzi huo utakaovishirikisha pia vyama vya
upinzani.
Msimamo
huo wa Pinda umekuja siku chache baada ya jina lake kukatwa katika
kinyang’anyiro cha urais ndani ya CCM hivi karibuni mjini Dodoma.
Pinda alikuwa kati ya wanachama 38 wa CCM waliojitosa katika kinyang’anyiro cha urais kwa tiketi ya chama hicho.
Hata
hivyo, jina lake lilikuwa miongoni mwa majina yaliyokatwa kwa mara ya
kwanza na kubakia matano ambayo yalipelekwa kwenye Kamati Kuu (CC) ya
CCM.
Majina
yaliyopelekwa kwenye kamati hiyo yalikuwa ni ya Waziri wa Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Ujenzi, Dk. John
Magufuli, Dk. Asha-Rose Migiro, Balozi Amina Said Salum na January
Makamba.
Majina hayo yalipelekwa Halmashauri Kuu (Nec) ya CCM ambapo wajumbe wake walipitisha majina matatu kati ya matano.
Waliopenya
katika kinyang’anyito hicho ni Dk. Magufuli, Dk. Migiro na Amina na
kupelekwa mbele ya Mkutano Mkuu na wajumbe kupiga kura na kumpata Dk.
Magufuli atakayepeperusha bendera ya chama hicho kumtafuta Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Pinda
aliteuliwa kushika wadhifa wa Uwaziri Mkuu na Rais Jakaya Kikwete, baada
ya aliyekuwa akishikilia wadhifa huo, Edward Lowassa, kujiuzulu baada
ya kuhusishwa na kashfa ya Richmond mwaka 2007.
CHANZO: NIPASHE
Chapisha Maoni