
1)
Taarifa nyingine ya CAG imetoka, kwa mujibu wa Katiba ya JMT na kwa
mujibu wa sheria za nchi. Taarifa hii imechelewa kutolewa kulingana na
mabadiliko ya Ratiba za Bunge ambapo hapo awali taarifa ilikuwa ikitoka
mwezi Aprili na kuwezesha kuchangia katika mchakato wa Bajeti ya nchi.
Taarifa ya mwaka huu na ile ya mwaka Jana imetoka wakati wa Bunge la
Bajeti na hivyo Bajeti ya Serikali haijazingatia hoja za ukaguzi ili
kuboresha mfumo wa matumizi ya fedha za umma. Ni vema utaratibu wa
zamani wa ripoti kutolewa mwezi Aprili urejewe ili wabunge waweze
kutumia ripoti hizo wakati wa kamati katika kujadili makadirio ya Bajeti
za Wizara mbalimbali.
2)
Taarifa kama miaka iliyopita bado sio nzuri. Mapato mengi ya Serikali
bado yanapotea. Uk. 53 wa Taarifa unaonyesha kuwa mizigo inayoingizwa
nchini kupita kwenda nchi jirani zinazotumia bandari zetu hubakia nchini
na kuingizwa sokoni hivyo kukwepa kodi. Mwaka 2013/2014 mizigo ya
transit iliyobaki nchini kiudanganyifu ilikuwa zaidi ya bidhaa 6000 kwa
mujibu wa Taarifa ya CAG. Hivyo kodi ya tshs 836 bilioni haikulipwa kwa
mizigo hiyo sawa sawa na 10% ya makusanyo yote ya kodi za ndani. Tshs
836 bilioni ilipotea mwaka 2013/14 peke yake. Wakati hili linatokea
Serikali ipo ukata mkubwa na kushindwa kuendesha miradi yake mbalimbali.
Fedha iliyokwepwa idara ya forodha peke yake inalipa Madeni yote ya
wakandarasi wa barabara wanaoidai TANROADS na riba kulimbikizwa kila
mwaka. Fedha hii ingelipa Madeni yote ya mfuko wa PSPF wanayoidai
Serikali. Fedha hizi zingeweza kulipia miradi 2 mikubwa nchini ya BVR na
vitambulisho vya Taifa ambayo inasuasua kutokana na ukata.(P.T)
Natoa
wito kwa CAG kwanza kuweka wazi orodha ya bidhaa hizo zilizobakia nchini
na kuingizwa nchini bila kulipa kodi. Vile vile CAG aweke wazi
wafanyabiashara wote walioagiza bidhaa hizi na vyombo vya kiuchunguzi
vichukue hatua za kuwashtaki wafanya biashara hawa mara moja.
Natoa
wito kwa Kamati ya Bunge ya PAC kuwaita mara moja maafisa wa TRA
kujieleza mbele ya kamati kuhusu suala hili na kuandaa taarifa maalumu
bungeni ili kuanika uoza huu unaopoteza mapato mengi sana ya Serikali.
3) CAG
kaonyesha kuwa kuna ubadhirifu mkubwa sana kitengo cha maafa cha ofisi
ya Waziri Mkuu ambapo tshs 163 billioni za chakula cha maafa
hazikukusanywa katika kipindi cha miaka 5 iliyopita. Huu ni kama mrija
wenye wastani wa tshs 32 bilioni kuchotwa kwa kisingizio cha chakula cha
maafa kwa wananchi. Kwa malezo ya CAG ni kwamba Watumishi wa Ofisi ya
Waziri Mkuu wamekula fedha za chakula cha misaada. Maana hakuna
uthibitisho wa kuwa mahindi yaliyogawanywa na taarifa kutolewa na Wakala
wa Akiba ya Chakula (NFRA). Kitengo cha maafa ofisi ya PM kimekuwa
mrija wa wizi wa fedha za umma, wizi ambao umekuwa ukifanyika bila ya
kugunduliwa kwa miaka 5 sasa. ACT Wazalendo inaisihi Kamati ya Bunge ya
PAC kufanya uchunguzi maalumu kwenye kashfa hii ya tshs 163 bilioni
katika Ofisi ya Waziri Mkuu na Wakala wa Hifadhi ya Chakula ( NFRA).
4) ACT
Wazalendo inalitaka Bunge kuchukua stahiki dhidi ya Wizara ya Ujenzi
kufuatia ripoti ya CAG kuonyesha kuwa Wizara ilidanganya Bunge katika
kupitisha Bajeti ya tshs 252 bilioni ambapo kati yake tshs 87 bilioni
ziliibiwa au matumizi yake kutoeleweka.
5) ACT
Wazalendo inampongeza CAG kwa kuendelea na zoezi la kisheria la kukagua
mahesabu ya vyama vya siasa. Hii inaweka misingi ya uwajibikaji kuanzia
kwenye vyama vya siasa, taasisi muhimu sana katika ujenzi wa demokrasia.
Vyama vya siasa vichukulie ripoti ya CAG kama changamoto ya kutoa
kwanza kibanzi kwenye macho yao ili kuwa na ' moral standing' ya
kupambana dhidi ya ubadhirifu wa fedha za umma nchini.
Zitto Kabwe
Kiongozi wa Chama ACT Wazalendo
Kiongozi wa Chama ACT Wazalendo
Chapisha Maoni