Takriban vijana 85 waliokuwa wamepokea mafunzo yenye itikadi kali wamejisalimisha kwa polisi nchini Kenya.
Msemaji wa Serikali imesifu hatua ya vijana hao, akitaja kuwa itachangia pakubwa ukusanyaji wa taarifa za kijasusi.
Awali vijana hao walihofia kujisalimisha kwa hofu kuwa wangetengwa katika jamii na hata kufungwa gerezani.
Maafisa katika wizara ya mambo ya ndani wamesema kuwa vijana hao walikuwa kati ya umri wa mika ishirini na thelathini.
Serikali ya Kenya iliahidi kuwasamehe vijana hao mapema mwezi uliopita, kufuatia uvamizi katika chuo kikuu cha Garissa, ambapo zaidi ya watu 150 waliuawa.
Kundi la wapiganaji wa Kiislamu wa Al Shabaab walikiri kutekeleza shambulizi hilo ambalo limepelekea chuo hicgo kufungwa.
Kujasalimisha kwa vijana hao kumepiga jeki juhudi za serikali ya Kenya dhidi ya mafunzo ya itikadi kali, yanayochangia hatua ya vijana hao kujiunga na makundi ya kivita kama vile Al Shabab.
Kundi hilo kutoka Somalia linaaminika kuwa na wafuasi nchini Kenya ambapo limetekeleza mashambulizi kadha katika jitihada ya kuilazimisha serikali ya Kenya kuondoa majeshi yake nchini Somalia.
Majeshi ya Kenya ni miongoni mwa kikosi cha kulinda amani cha muungano wa Afrika Amisom ambao wanaisaidia serikali dhaifu ya Somalia kupigana na waasi wa Al Shabaab.
Chapisha Maoni