Waandamanaji wanaopinga kauli ya Nkurunziza ya kutaka kuwania muhula wa tatu
Rais wa Burundia Pierre Nkurunziza amehairisha uchaguzi wa ubunge kwa siku kumi hayo yamesemwa na Msemaji wa Rais Willy Nyamitwe kwa shirika la habari la AFP kuwa kufuatia jaribio la mapinduzi juma lililopita na vurugu zilizofuatia ni bora kuahirisha uchaguzi wa Ubunge .
''Uchaguzi huo wa ubunge ulikuwa umeratibiwa kufanyika tarehe 26 Mei lakini sasa inatubidi kuihairisha ili kuwasikiza washirika wetu wa kimataifa pamoja na tume ya uchaguzi ambayo pia inatumia muda huo kutatua maswali yaliyoulizwa na vyama vya upinzani.'' alisema Nyamitwe.
Nyamite ameongeza kuwa, uchaguzi wa Urais uliopangwa kufanyika 26 Mei bado haijabadilika.
''Subiri tu'' Nyamitwe aliwaambia waandishi wa habari.
Mwandishi wa BBC aliyeko huko Ruth Nesoba amesema kuwa tayari rais Nkurunziza ametia sahihi amri hiyo ya kuhairishwa kwa uchaguzi ambapo Umoja wa mataifa ya bara Ulaya EU, na Umoja wa mataifa ya Afrika AU, yametoa wito kwa uchaguzi huo uliokumbwa na utata mkubwa uhairishwe ilikutoa fursa kwa mazungumzo ya upatanishi kuendelea .
Hapo jana Rais wa Afrika Kusini alitilia pondo hoja hiyo ya kuahirisha uchaguzi akisema ni bora uchaguzi huo uliopangwa ''uhairishwe''. Hadi sasa Takriban watu 20 wameuawa kufuatia makabiliano baina ya polisi na waandamani katika mji mkuu wa Bujumbura kilele ikiwa ni juma lililopita makamanda waasi walipotangaza jaribio la mapinduzi rais Nkurunziza akiwa mjini Dar es Salaam kuhudhuria mkutano wa viongozi wa kanda uliolenga kutatua mzozo wa kisiasa nchini mwake.
Wapinzani wa rais Nkurunziza wanasema kuwa kutangazwa kwake nia ya kuwania muhula wa tatu unakiuka sheria na makubaliano ya amani ya mwaka wa 2006 yaliyomaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka 13. Nkurunziza kwa upande wake anashikilia kuwa ana haki ya kuwania muhula mwengine kwani muhula wa kwanza hakuchaguliwa na wanainchi bali wabunge.
Takriban watu laki moja wamekimbilia mataifa jirani wakihofia kutibuka upya kwa mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.
Chapisha Maoni