Ndivyo
alivyosema na bila shaka ndivyo anavyoamini Waziri Mkuu wa zamani,
Edward Lowassa, lakini kauli ambazo amekuwa akizitoa tangu kuanza kwa
mbio za urais zinamuweka katika hali ngumu Mwenyekiti wake, Rais Jakaya
Kikwete.
Lowassa
alirudia moja ya kauli hizo juzi alipokuwa Dar es Salaam kuendelea na
kazi ya kutafuta wadhamini aliposisitiza kauli ya Baba wa Taifa Mwalimu
Julius Nyerere kuwa “Watanzania wanataka mabadiliko, wasipoyapata ndani
ya CCM watayatafuta nje,” akisisitiza kuwa yeye ndiye anayeweza kuleta
mabadiliko hayo.
Mbunge
huyo wa Monduli ametoa kauli hizo kabla ya vikao vya juu vya kufanya
uamuzi wa mgombea urais wa CCM vitakavyoongozwa na Rais Kikwete. Vikao
hivyo vitaanza Julai 8.
Tayari
makada 42 wamejitokeza kuchukua fomu za kuomba ridhaa ya chama hicho
kikongwe kugombea urais na kutoa ahadi mbalimbali, lakini Lowassa,
ambaye amekuwa akipata wadhamini wengi kuliko makada wengine, ndiye
ambaye ametoa kauli zinazomuweka Kikwete kwenye hali ngumu.
Tangu
alipoanza kuzungumzia urais kwenye kikao cha kwanza na wahariri Mei 25
mjini Dodoma, Lowassa amekuwa akitoa kauli kadhaa katika mikoa
mbalimbali nchini, akianzia Arusha ambako alitangaza nia ya kugombea
urais kwa tiketi ya CCM na baadaye kwenye harakati za kusaka wadhamini.
Asiyenipenda ahame CCM
Akijibu
swali kwamba anaweza kuhama chama iwapo jina lake litakatwa kwenye
mchakato wa ndani ya CCM, Lowassa alieleza jinsi alivyokitumikia chama
na imani yake.
“Sina
mpango wa kuhama chama changu, sina Plan B. Mimi ni Plan A tu. Tangu
nimalize chuo kikuu mwaka 1977, nimekuwa mwana-CCM. Sijafanya kazi nje
ya CCM ukiondoa miaka ambayo nilikuwa vitani Uganda na nilipohamishiwa
Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha. Maisha yangu yote ni CCM,”
alisema Lowassa.
“Kama kuna mtu ambaye hanitaki ndani ya CCM, yeye ndiyo ahame, siyo mimi.”
Safari hii JK ataniunga mkono
Akihutubia
maelfu ya wananchi kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Mei 30 wakati
akitiania, Lowassa alielezea tukio la kuchukua fomu za kuomba ridhaa ya
CCM kuwania urais mwaka 1995 wakati alipofanya mkutano na waandishi wa
habari akiwa pamoja na Kikwete, ambaye pia alichukua fomu hizo.
“Wakati
ule sote tulikuwa wanasiasa vijana. Pamoja tulikwenda kuchukua fomu na
baadaye kwa pamoja tukazungumza na waandishi wa habari. Tulileta hamasa
kubwa pale tulipofanya jambo ambalo halikuzoeleka kwa Watanzania kwa
kutangaza kwamba yeyote atakayepita kati yetu, mwenzake ambaye
hangefanikiwa angemuunga mkono mwingine,” alisema Lowassa na kuongeza
kuwa wakati ule alimuunga mkono Kikwete...“Natarajia safari hii, Kikwete
ataniunga mkono.”
Mwaka
huo, Kikwete alishindwa na Benjamin Mkapa ambaye baadaye akawa Rais wa
Serikali ya Awamu ya Tatu. Mwaka 2005, Lowassa hakuchukua fomu na badala
yake alimuunga mkono Kikwete aliyeshinda na mbunge huyo wa Monduli
kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya Awamu ya Nne.
Pengine
kauli hiyo ya Lowassa kutaka amuunge mkono ndiyo iliyosababisha Rais
Kikwete kutupiwa swali na mwanadiplomasia wa Marekani Juni 9 wakati
akizungumza na Jumuiya ya Watanzania waishio Uholanzi katika hoteli ya
Chawnie Plaza. Rais Kikwete alijibu kuwa hana mtu wake na kwamba wote ni
wagombea wake, na kama ni suala la kuchagua, ana kura moja tu kama
wajumbe wengine.
Mabadiliko aliyotabiri Nyerere
Akiwa mjini Iringa Juni 20, Lowassa alitumia kauli hiyo ya Nyerere kuhusu mabadiliko ndani na nje ya CCM.
“Baba wa
Taifa alisema kuwa Watanzania wanahitaji mabadiliko na wasipoyapata
ndani ya CCM watayatafuta nje ya CCM,” alisema Lowassa.
“Huu ni
wakati wa mabadiliko. CCM ikijipanga inaweza kuleta mabadiliko na mtu wa
kuleta mabadiliko hayo ni mimi,” alisema Lowassa kwenye Uwanja wa
Samora mjini Iringa.
Pia
aliwaambia wahariri mjini Dodoma kuwa hawezi kuondoka CCM na kama kuna
watu wanadhani hivyo, waondoke wao. Alikuwa akijibu swali kama atakuwa
tayari kuondoka CCM iwapo ataenguliwa kwenye mchujo wa wagombea urais.
Hakuna wa kumkata jina
Juni 22,
akizungumza mara baada ya kuwasili mkoani Ruvuma alisema hatarajii jina
lake kukatwa katika vikao vya CCM vitakavyoketi kumteua mwanasiasa
atakayepeperusha bendera ya chama hicho katika kinyang’anyiro cha urais.
“Nimekuwa
mwanaCCM tangu mwaka 1977 nilipomaliza chuo kikuu, sijawahi kufanya
kazi nje ya CCM hivyo nakijua chama na hakuna mgombea atakayeweza
kuvunja rekodi ya utendaji wangu katika chama, sasa leo anayetaka kukata
jina langu anatoka wapi? Anakata kwa sababu gani? Sioni kosa la kukatwa
jina na Watanzania hawaoni, kwa hiyo msiwe na wasiwasi jina litarudi
tu,” alisema Lowassa.
Anayemtuhumu kwa ufisadi amtaje
Siku ya
kuchukua fomu Juni 5, Lowassa alijibu kwa kifupi maswali ya wanahabari
na kusema kama kuna mtu ana ushahidi wa tuhuma za ufisadi dhidi yake
amtaje jina.
Chapisha Maoni