0
 
Mke wa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, Janeth Pombe.

KUMEKUCHA! Siku chache baada ya Waziri wa Ujenzi, Dk. John Pombe Magufuli kuteuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa mgombea urais kupitia chama hicho, mkewe, Janeth Pombe amechambuliwa vilivyo na walimu wenzake, Amani lina kila kitu.
Juzi, Amani lilifika Shule ya Msingi Mbuyuni, Oysterbay jijini Dar ambayo Janeth amekuwa akifundisha na kufanikiwa kuzungumza na mwalimu mkuu wa shule hiyo na walimu wengine.
MWALIMU MKUU AANZA



Akizungumza na gazeti hili, mwalimu mkuu wa shule hiyo, Doroth Malecela (John Malecela anamwita baba mdogo) alisema:

“Kwetu sisi kama shule, tunajivunia kwa sababu hata mke wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete, mama Salma Kikwete alifundisha shule hii.

AOMBA MAGUFULI ASHINDE “Kama John Magufuli atafanikiwa kuingia madarakani, taifa linatakiwa kujua Mbuyuni ndiyo shule inayotoa marais wetu kupitia wake zao.



“Hivi sasa tunaomba uchaguzi uende vizuri, Magufuli ashinde ili naye tumlee. Mbali na yote, lakini pia kuondoka Janeth kutatuachia pengo kwetu maana tulikuwa naye kwa kipindi chote lakini ni wazi kwamba kama mumewe atashinda urais, kisheria yeye Janeth hataweza kuendelea kufundisha tena hapa,” alisema mkuu huyo wa shule.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mbuyuni, Dar.

MAISHA BINAFSI

Mwalimu Doroth alimchambua Janeth Pombe (jina analotumia) kuwa, katika mazingira ya shuleni, mwalimu huyo aliishi kama walimu wengine na si kama mke wa waziri kwa sababu hajikwezi. Hata mavazi yake ni simpo tu.

“Kwanza Janeth ni mcheshi, lakini pia ni mpole na mchapakazi. Ni mtu wa kujichanganya na wengine kwenye shida na raha. Kwenye furaha hakusita kuonesha uchangamfu wake hata kwa kucheza. Kila mmoja alipenda uwepo wake,” alisema mwalimu huyo.

Wanafunzi wa Shule ya Msingi Mbuyuni ya jijini Dar.

MASOMO ANAYOFUNDISHA

“Hapa anafundisha wanafunzi wa darasa la tano masomo ya Uraia, Historia na Jiografia.”

KUHUSU UCHELEWAJI

“Hapana, kwa kufuata taratibu za kazi na sheria za shule, mwalimu Janeth alikuwa akifika mapema na kuanza majukumu yake bila kupoteza muda.”

USAFIRI ANAOUTUMIA

“Amekuwa akiletwa kazini muda mwafaka na gari na dereva wake na muda wa kutoka pia alifuatwa kwa gari bila aina yoyote ya mbwembwe.”

Kibao cha Shule ya Msingi Mbuyuni.

HAKUWA MTORO?

“Inapotokea ana udhuru wa kumfanya ashindwe kuhudhuria shuleni amekuwa akitoa taarifa mapema kwa uongozi. Kifupi alikuwa mtiifu, hakuringia cheo cha mumewe hata siku moja na haikuwa rahisi mtu kumjua kuwa ni mke wa Waziri John Magufuli bila kuambiwa.

KUHUSU FAMILIA

“Pamoja na kuwa mume wake ni waziri, watoto wao wote wamesoma katika shule hii. Kuanzia darasa la kwanza mpaka la saba na walikuwa wakishirikiana na wanafunzi wenzao.

“Mtoto wao wa mwisho alimaliza hapa mwaka jana, sasa anasoma Shule ya Sekondari ya Kata ya Oysterbay na kuna muda huwa anakuja kutusalimia,” alisema mwalimu mkuu huyo.

SHEMEJI UNATUACHAJE

“Kuna kipindi walimu tulisema JK unatuachaje shemeji yetu (kwa ajili ya mama Salma), lakini alitujibu atakuja shemeji yenu mwingine. Kwa usemi ule sasa tunaamini, shemeji yetu anaweza kupatikana tena.”

SIRI YA SHULE

Akieleza sababu inayoifanya shule yao kuibua wake wa marais (kama Magufuli atashinda) mwalimu huyo alisema:

“Hakuna siri kubwa, huku Oysterbay, Masaki ndo’ wanakoishi vigogo wa serikali hivyo huwa ni rais wake zao kufundisha kwenye shule hii.”

ANAIJUA SIASA?

“Mama Magufuli yeye mara kwa mara husifia kazi yake ya ualimu, sikuwahi kumsikia akisema anapenda siasa hayupo huko kabisa.”

Waandishi: Mayasa Mariwata na Shani Ramadhani.

Chapisha Maoni

 
Top