Na Daudi Manongi-MAELEZO.
Tanzania inategemea kupata Megawati 400
za umeme kutoka Ethiopia ikiwa ni moja ya makubaliano yaliyofikiwa baada
ya ziara ya kikazi ya siku mbili ya Waziri Mkuu wa Ethiopia Mhe.Haile
Mariam Desalegn.
Hayo yamesemwa na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt John Pombe Magufuli alipokuwa akizungumza
na vyombo vya habari juu ya makubaliano na mikataba ambayo nchi za
Tanzania na Ethiopia wametiliana saini Ikulu Jijini Dar es Salaam.
“Tukitaka kujenga uchumi wa viwanda ni
lazima tuwe na umeme wa kutosha,wenzetu Ethiopia wametuonyesha njia na
mimi nimemuomba Mhe.Waziri atusaidie wataalamu kutoka nchini kwake ili
waje tuwaonyeshe maeneo mbalimbali watusaidie katika kupata umeme wa
uhakika kwa kujenga mabwawa ya umeme ambayo yamesaidia sana katika
kupatikana kwa umeme wa kutosha nchini kwao.”Aliongeza Rais Magufuli.
Aidha amesema kuwa kupatikana kwa umeme
huo kutasaidia kuleta changamoto kwa shirika la umeme nchini katika
kuwapatia wananchi bei ya chini na hivyo kuleta ushindani katika
upatikanaji wa umeme nchini.
Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Ethiopia
Mhe.Haile Mariam Desalegn amesema kuwa wana mengi ya kujifunza kutoka
Tanzania kwani nchi hizi mbili zina historia inayofanana na kuongeza
kuwa hakuna haja ya wao kwenda nje ya Afrika kupata uzoefu katika
masuala mbalimbali.
Ameongeza kuwa lengo kuu la kuja nchini
ni kwa sababu anahamini nchi hizi mbili zinaweza kuunganisha nguvu zake
na kuwa nguzo kuu katika maendeleo katika eneo la ukanda wa Afrika
Mashariki na kati.
“Tanzania na Ethiopia ni nchi ambazo
zina ushirikiano mzuri sana,sisi sio washindani bali tunasaidiana katika
masuala mbalimbali kwani tumekuwa katika hatua mbalimbali za kuwaondoa
wananchi wetu katika umaskini katika hatua zinazofanana,na huu ni wakati
muafaka katika kuimarisha ushirikiano wetu kwa faida ya watu wetu kwa
ujumla”Alisisitiza Mhe.Desalegn.
Aidha amesema kuwa mabadiliko ya
kilimo katika nchi zetu ndio msingi wa maendeleo pamoja na
utumiaji wa teknolojia bora utasaidia katika maendeleo ya viwanda
vidogo vidogo.
Viongozi hawa wamekubaliana kushirikiana
kwa kubadilishana uzoefu juu ya namna sekta mbalimbali zitakavyoleta
manufaa ya kiuchumi zikiwemo huduma za benki, madini na gesi, elimu na
mawasiliano.
Ziara ya Waziri Mkuu Mhe. Haile Mariam
Dessalegn imekuwa ya manufaa makubwa kwa Tanzania na amesisitiza kuwa
wakati umefika wa kukuza biashara kati ya nchi hizi ambazo kwa sasa
thamani ya biashara kati yake ni Dola za Marekani milioni 2.24 tu.
Chapisha Maoni